ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 19, 2020

WATUHUMIWA 58 VURUGU PEMBA WAKAMATWA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia), akimsikiliza mmoja wa majeruhi wa vurugu za kisiasa zilizotokea Visiwani Pemba, ambapo jumla ya majeruhi saba wanapatiwa huduma katika Hospitali ya Micheweni iliyopo Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Na Mwandishi Wetu

Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar linawashikilia watuhumiwa 58 wa vurugu zinazodaiwa kuhusisha itikadi za kisiasa huku wananchi saba wakijeruhiwa katika tukio hilo lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la Kwale Wilaya ya Micheweni Pemba

Akizungumza leo na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba , Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohammed Haji Hassan amesema Jeshi la Polisi linaendelea na kazi yake ya msingi ya kulinda amani katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu na halitamvumilia mtu yoyote atakaekiuka kanuni na sharia wakati huu ambapo nchi inahitaji amani na utulivu ili wananchi waweze kupiga kura.

“Jeshi la Polisi linaendelea na msako usiku na mchana kukamata watu wote waliohusika na tukio hilo,jumla ya watuhumiwa 58 wanashikiliwa na hatua za kisheria zinaendelea,natoa wito kwa yoyote ataekajaribu kuvuruga amani hatua kali zitachukuliwa bila hofu bila kufumba macho kuhakikisha amani inaendelea kuwepo” Alisema CP Mohammed

Akizungumza baada ya kuwatembelea majeruhi hao Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amelipongeza Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kwa kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia suala hilo huku akiwataka wananchi kutii sheria za nchi ili kuepusha machafuko kuelekea Uchaguzi Mkuu.

“Naomba kuchukua fursa hii kuwanasihi wananchi kuepuka kuchochewa kuvunja sheria za nchi kuelekea katika uchaguzi na serikali imejipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi unakua wa salama na amani” alisema Masauni

Jumla ya majeruhi saba wamelazwa katika Hospitali ya Micheweni huku Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk.Mbwana Shoka akiweka wazi kuimarika kwa afya zao baada ya kupata majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti majeruhi wa tukio hilo wameiomba serikali kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha uchaguzi visiwani humo ili kuepusha machafuko yatakayopelekea kuhatarisha maisha ya wananchi.

No comments: