Advertisements

Tuesday, October 27, 2020

Watumiaji wa Mtandao Wamtabiria Ushindi Magufuli



HUKU ikiwa imesalia siku moja Watanzania kupiga kura za kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani, baadhi ya Watanzania wanaotumia mtandao wa intaneti wamemtabiria ushindi Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Pombe Magufuli, na hii ni kwa mujibu wa kura ya maoni inayoendeshwa na tovuti maarufu ya kurayamtandaoni.com.

Takwimu za tovuti hiyo zinaonyesha kuwa, mpaka kufikia muda wa gazeti hili kwenda mitamboni hapo jana majira ya alasiri, jumla ya watu 35,689 walikuwa tayari wamepiga kura ya maoni katika mtandao huo, huku Dkt. Magufuli akipata kura 26,719 sawa na asilimia 74.87. akifuatiwa na Mgombea wa CHADEMA, Tundu Lissu mwenye kura 5,999, sawa na asilimia 16.81.

Tanzania inaingia katika Uchaguzi Mkuu wa 6 wa vyama vingi, tangu kuanza kwa mfumo huo mwezi Julai mwaka 1992. Mvutano mkubwa katika uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuwa kati ya vyama vya CCM na CHADEMA.

Dkt John Magufuli anagombea muhula wa pili, akijinadi kwa kazi ya miaka mitano ya awali katika kuboresha miundombinu, upatikanaji wa umeme vijijini, afya, mabadiliko katika sekta ya elimu, nidhamu katika utumishi wa umma na matumizi serikali.

Mgombea wa CHADEMA Wakili Tundu Lissu ambaye amekuwa nchini Ubelgiji kwa kipindi kirefu akipata matibabu toka aliposhambuliwa kwa risasi mjini Dodoma, anajinadi kwa kauli mbiu ya maendeleo, haki na uhuru wa watu.

Mtindo wa kura ya maoni kwa njia ya mtandao umekuwa kwa kasi sehemu nyingi duniani hasa kutokana na matumizi ya mtandao wa intaneti kuongezeka miaka ya karibuni.

Wanasayansi wengi wa siasa wanaamini kura ya maoni ya mtandao yenye sampuli yenye uwakilishi sahihi hutoa mwelekeo wa picha halisi ya matokeo ya chaguzi.

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) za hadi kufikia Juni 2020 zinaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya watumiaji wa intaneti wapatao 27,100,146.

Uchaguzi Mkuu Tanzania mwaka huu una jumla ya Wagombea Urais 15. Takwimu za Tume ya Uchaguzi (NEC) zinaonesha kuwa Tanzania ina wapiga kura 29,188,347, vituo vya kupigia kura 80,155 ambapo kwa Tanzania Bara kuna vituo 79,670 na kwa upande wa Zanzibar kuna ituo 1,412, hii ikiwakilisha idadi ya wapigakura 500 kwa kila kituo.

Iwapo watumiaji wa intaneti wamebashiri sahihi au la kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu, ni suala la kusubiri kuona.

Na Sagati Chacha

No comments: