Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungunza kwenye mkutano wa kanda wa uwekezaji katika sekta ya Mazao ya Bustani (Horticulture) uliyofanyika Disemba 5, 2020 kwenye Hoteli ya Hyat Regency, Jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea na Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Wazalishaji wa Mbogamboga na Matunda Tanzania (TAHA) Mhandisi Zebadiya Moshi, wakati wa mkutano wa kanda wa uwekezaji katika sekta ya Mazao ya Bustani (Horticulture) uliyofanyika Disemba 5, 2020 kwenye Hoteli ya Hyat Regency, Jijini Dar es salaam. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Abubakar Kunenge, Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Wazalishaji wa Mbogamboga na Matunda Tanzania (TAHA) Mhandisi Zebadiya Moshi na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akiongea na wadau wa sekta ya mazao ya bustani (Horticulture) wakati wa mkutano wa kanda wa uwekezaji katika sekta hiyo Disemba 5, 2020 Jijini Dar es salaam, kwenye Hoteli ya Hyat Regency, Jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Wazalishaji wa Mbogamboga na Matunda Tanzania (TAHA) Mhandisi Zebadiya Moshi akimkabidhi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa taarifa ya changamoto zilizopo katika kilimo cha Mbogamboga, Disemba 5, 2020 Jijini Dar es salaam, kwenye Hoteli ya Hyat Regency, Jijini Dar es salaam.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema tasnia ya kilimo cha mazao ya bustani ina mchango mkubwa kwenye maendeleo ya uchumi nchini na kuajiri watu zaidi ya milioni nne, hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na wafanyabiashara wengi.
Kufuatia umuhimu wa tasnia hiyo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, Waziri Mkuu ameaiagiza Wizara ya kilimo ianzishe Mamlaka ya Horticulture na Kituo cha Utafiti kwa ajili ya kusimamia na kuratibu mazao ya matunda, viungo na mbogamboga tu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Desemba 5, 2020) baada ya kufungua Kongamano la Kikanda la Biashara la Uwekezaji katika Tasnia ya Mazao ya Bustani lililofanyika kwenye Hoteli ya The Kilimanjaro Hyatt Regency, jijiji Dar es Salaam.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita uzalishaji wa mazao ya bustani nchini uliongezeka kwa asilimia 10.5 kutoka tani 5,931,900 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 6,556,102 mwaka 2018/2019.”
Amesema takwimu hizo zinathibitisha ukuaji wa tasnia hiyo na uwepo wa haja ya kuweka mikakati ya kuiendeleza zaidi. “Hivyo basi, kwa kuwa bei kwa tani inakadiriwa kuwa shilingi 500,000 thamani ya mazao ya kilimo cha mazao ya bustani kwa mwaka 2018/2019 inakadiriwa kuwa kiasi cha shilingi trilioni 3.3.”
Waziri Mkuu amesema mbali na kuchangia katika ukuaji wa uchumi, tasnia hiyo inasaidia kujenga Taifa lenye watu wenye afya nzuri, nguvu na uwezo wa kufanya kazi, pia ni chanzo kikuu cha lishe na afya bora kwa Watanzania kutokana na virutubisho vingi kwa ulaji wa mbogamboga, matunda na viungo.
Amesema mazao ya bustani yamekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na gonjwa hatari la Covid-19 kwa sababu dawa mbadala za asili zilizosaidia wananchi wengi duniani kote kudhibiti ugonjwa huo zilitokana na matunda na viungo.
“Kutokana na vilelezo hivyo, ni wazi kuwa mchango wa tasnia ya kilimo cha mazao ya bustani kwenye maendeleo ya watu na uchumi wa nchi yetu na dunia kwa ujumla ni mkubwa na iwapo fursa zilizopo zitafanyiwa kazi, basi safari yetu ya kuelekea kwenye uchumi ulio imara zaidi itakuwa ya mafanikio makubwa, kwa kipindi kifupi.”
Wakati Huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ili kuwezesha biashara hususan ya mazao yanayoharibika haraka kama mazao ya bustani, minofu ya samaki na nyama, Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025, imepanga kununua ndege ya mizigo kwa kuzingatia mahitaji ya biashara na ukuaji wa uchumi.
“Pamoja na ndege ya mizigo tutanunua ndege kubwa mbili za masafa marefu na ndege mbili za masafa ya kati ili kuongeza fursa za biashara. Pia Serikali imeunda kamati maalum inayojumuisha wataalamu wa Serikali na wale wa sekta binafsi, ambayo imeanza kuainisha changamoto za usafirishaji na za kimfumo katika bandari na viwanja vyetu vya ndege ili kufanya maboresho yanayohitajika na hivyo tuweze kutumia miundombinu ya ndani katika kusafirisha bidhaa zetu.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagiza taasisi zote zinazohusika na usafirishaji wa mizigo kwa njia ya anga na bahari pamoja na kamati iliyoundwa kusimamia zoezi hilo zifanyie kazi kwa haraka mapendekezo ya wataalamu yatakayotokana na utafiti unaoendelea kuhusu kuboresha miundombinu na mifumo ya usafirishaji.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya alisema kutokana na umuhimu wa tasnia hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa zao hilo wameendelea kufanya uchambuzi wa athari za wadudu kwa ajili ya baadhi ya masoko mapya kama China, India na Afrika Kusini.
Pia, Bw. Kusaya alisema kutokana na umuhimu wa tasnia hiyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo ili iendelee kutoa mchango mkubwa katika Taifa na hivyo kuwezesha ukuaji wa uchumi, ajira na upatikanaji wa malighafi za viwandani
No comments:
Post a Comment