Saturday, January 30, 2021

NAIBU WAZIRI KUNDO ATOA WITO KWA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Andrea Kundo (katikati) akifungua baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na kulia ni Naibu wake Dkt Jim Yonazi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab Chaula (kulia) akizungumza katika baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, anayefuata ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Andrea Kundo akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Jim Yonazi.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Andrea Kundo (kushoto) akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Jim Yonazi katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakifuatilia kwa karibu mkutano wa baraza hilo ulilofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Na Faraja Mpina – WMTH

Wito umetolewa kwa wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa kuzingatia vigezo walivyojiwekea.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Andrea Kundo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo jijini Dodoma,ambapo amesema ili kutekeleza malengo ya wizara hiyo , ushirikiano wa hali ya juu unahitajika miongoni mwa viongozi wa wizara, watumishi na wadau wa sekta ya mawasiliano kwa ujumla.

Aidha,Menejimenti ya wizara hiyo imetakiwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri na wezeshi ya utendaji kazi,mahusiano bora kazini pamoja na wafanyakazi kupata stahiki zao kwa muda muafaka na pale inaposhindikana taarifa sahihi zitolewe kwa wakati husika.

Aliongeza kuwa, kila mtumishi anatakiwa kusoma na kuelewa sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Kazi ya baraza la wafanyakazi ni kuangalia haki za wafanyakazi na utekelezaji wa wajibu wao, kwasababu haki na wajibu vinaenda sambamba”, Kundo

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainabu Chaula amesema kuna mafanikio yako mengi kupitia baraza hilo hasa katika kujenga nidhamu na utendaji wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

Aliongeza kuwa , mkutano huo unajadili utekelezaji wa majukumu na mipango ya Wizara kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020/2021, mapendekezo ya muundo mpya wa Wizara, kukumbushana kuhusu ujazaji wa fomu za kupima utendaji kazi (OPRAS) na kupokea taarifa za wafanyakazi kupitia wawakilishi wao

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Jim Yonazi amesema wanania ya dhati ya kuhakikisha kuwa sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari inakuwa mfano katika utendaji kazi kupitia umoja na mshikamano uliopo kama nguzo muhimu ya kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta mafanikio makubwa kwa sekta na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Laurencia Masigo amesema wao kama TUGHE watahakikisha wanahamasisha ushirikiano katika kufanya kazi kwa kujituma ili kutumiza malengo ambayo wizara hiyo imejiwekea.

Hata hivyo, Wajumbe wa Baraza hilo wamekumbushwa majukumu ya Baraza la wafanyakazi mahali pa kazi kuwa ni pamoja na kuwashirikisha wafanyakazi wote katika utekelezaji wa shughuli za wizara kwa ushirikiano na menejimenti lakini pia kuishauri wizara juu ya mambo muhimu yanayohusu maslahi na hali bora ya wafanyakazi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

No comments: