WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika kambi mpya ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, leo. Amesema askari watakaoshindwa kuwabaini Wahamiaji haramu hususani maeneo ya mipakani wanapoingilia watawajibishwa. Kulia ni Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela, na wapili kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tanga, baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ajili ya kufungua mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika kambi mpya ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga. Wanne kulia ni Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (aliyevaa suti), akiangalia ramani ya Kambi mpya ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, ambayo inaendelea kujengwa. Waziri huyo alifika kambini hapo kwa ajili ya kufungua mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika kambi hiyo. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika Kambi ya mpya ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ambaye alifungua mafunzo hayo.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (wapili kushoto) akitoka kukagua ujenzi wa jengo jipya la utawala la kambi ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela, na katikati ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia) akiweka jiwe la msingi la jengo la Utawala la kambi ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga. Wanne kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela, na watatu kushoto ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (katikati waliokaa), Mkuu wa Mkoa Tanga, Martine Shigela (wapili kulia), Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala (wapili kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, …..wakiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa kambi ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, baada ya hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika Kambi hiyo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Mwandishi Wetu, MOHA.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema askari watakaoshindwa kuwabaini Wahamiaji haramu hususani maeneo ya mipakani wanapoingilia watawajibishwa.
Waziri Simbachawene amesema kitendo cha wahamiaji haramu kukamatwa maeneo mbalimbali ndani ya nchi, ambayo siyo mipakani ni kutokana na kuwepo na mawakala wanaofanikisha wahamiaji hao kuingia nchini.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wa uhamiaji katika kambi mpya ya mafunzo ya Boma Kichaka Miba, iliyopo Wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, Simbachawene amesema watawashughulikia askari wote wanaoingia katika mkoa ya mipakani ambapo wanaingia kwa mara ya kwanza wahamiaji hao.
“Wahamiaji haramu kama tukiwakata Morogoro na wakasema wameingia hapa Mkinga, sisi hatushughuliki na wale Morogoro, tutashughulika na waliopo Wilayani Mkinga na Tanga, tuwahoji wamepitajepitaje wahamiaji hawa haramu,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Pia tutawauliza polisi, ilikuaje musiwaone wahamiaji hawa haramu maana ‘barrier’ zote zenu, hawa hawatembei kwa miguu, walipanda gari, walipandia wapi gari, na kama wakituambia walipanda gari, hawa watu wote (Askari Polisi na Uhamiaji) wapo kwenye Wizara yangu, wote nitafagia.”
Pia Waziri huyo amesema mipaka ya nchi lazima ilindwe kwasababu askari wanataaluma zote za kijeshi ya kupambana na wahamiaji haramu hivyo kitendo cha kupita mipakani na kukamatwa maeneo ya ndani ya nchi ni hatari na kama adui atakuwa ameishambulia nchi.
“Ukiona msafara wa wahamiaji haramu umefanikiwa kutoka point A mpaka B ujue kuna mawakala, kutoka point B mpaka C ujue kuna mawakala, wale watu wanaokuja ni wageni, wanawezaje kupita point A mpaka Point B, kama wamefanikiwa kufika mpaka Dar es Salaam wakakamatwa Tegeta au Mbezi, maana yake tumeshapigwa kama ni adui, lazima tuwe makini kila mtu katika eneo lake,” alisema Simbachawene.
Aidha, Simbachawene aliwataka wanafunzi wa Kambi hiyo kuzingatia masomo ya Kiuhamiaji wanayopewa yakiwemo ya uongozi na utawala, masuala ya kikonsula, mawasiliano, ulinzi wa kujihami na gwaride.
“Mafunzo mtakayoyapata kutoka kwa wakufunzi wenu yanalenga kudumisha nidhamu ya kijeshi, uzalendo, utii, uwajibikaji na maadili bora, ninawaomba zingatieni tunu hizo katika kipindi hiki chote cha mafunzo, kwani ndio silaha kubwa kwa askari na katika uongozi bora,” alisema Simbachawene.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI), Dkt. Anna Makakala, alisema mafunzo katika kambi huyo mpya, yanajumuisha jumla ya askari na maafisa wa uhamiaji 287, wanawake 81 na wanaume 206, ambapo mchanganuo wa kozi ya Mrakibu Msaidizi wapo 32, Mkaguzi Msaidizi wapo 112, kozi ya Sajini 42 na kozi ya Koplo wapo 101.
“Mheshimiwa mgeni rasmi napenda kukujulisha kuwa Kambi ya Mafunzo ya Boma Kichaka Miba inamilikiwa na Idara ya Uhamiaji na Chuo cha Kikanda (TRITA) kilichopo Mjini Moshi, kambi hii ina ukubwa wa ekari 395 na tayari tumekabidhiwa hati miliki, ujenzi wa kambi hii ulianza rasmi mwezi Julai, 2020 na kiasi kilichotumika ni shilingi milioni 140, fedha hizi zimetokana na michango ya hiari ya askari na maafisa wa Uhamiaji ambao walichangia Shilingi milioni 81 na wadau rafiki wa uhamiaji walichangia milioni 59 ikiwemo vifaa vya ujenzi” alisema Dkt. Makakala.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela aliwataka waishio jirani na kambi hiyo kutoa ushirikiano na kambi hiyo, na pia wasivamie maeneo ya kambi hiyo ya Uhamiaji wakaona vichaka wakafikiri ni eneo ambalo halina mwenyewe na wakavamia.
Mwisho/-
No comments:
Post a Comment