ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 17, 2021

SIMBA YAJA NA SAPRAIZI

SIMBA inakuja na sapraizi nyingine kimataifa. Kitendo chao cha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na ushindi murua ugenini dhidi ya AS Vita Club umeongeza uwezekano mkubwa wa kuwa na timu nne msimu ujao.

Kufanya vizuri kwa Simba katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, kwa kiasi kikubwa kutaiwezesha Tanzania kuwakilishwa na klabu nne katika mashindano ya klabu Afrika ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa mujibu wa mfumo wa ukokotoaji alama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), hadi sasa kabla ya kuanza kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania ina nafasi ya kuingiza timu nne kutokana na kuwepo katika kundi la nchi 12 ambazo kila mmoja ina fursa ya kuwakilishwa na timu nne.

Tanzania ipo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 15 ikichukua nafasi ya Libya ambayo iko nafasi ya 13 kwa idadi ya pointi 11 ilizonazo.

Pointi hizo zinaweza kuongezeka zaidi ikiwa Simba itamaliza angalau ikiwa nafasi ya tatu kwenye kundi au kufuzu robo fainali na hatua nyingine zaidi lakini kama itashika mkia kwenye kundi, mambo yanaweza kwenda tofauti kutokana na ushindani wa baadhi ya nchi ambazo zinanyemelea kuingia katika kundi hilo la nchi 12.

Libya timu yake ya Al Ahly Benghazi inaweza kuipiku Tanzania iwapo Simba haitofanya vyema kwenye makundi na yenyewe ikafika hatua za juu zaidi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Benghazi juzi imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya DC Motema Pembe katika uwanja wa nyumbani na kujiweka katika nafasi finyu ya kufuzu hatua ya makundi. Timu hizo zitarudiana wiki ijayo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kidao Wilfred alisema kuwa pamoja na kuona msimamo huo na sasa wanasubiri taarifa rasmi kutoka Caf.

“Nimeona msimamo wa sasa, siwezi kusema lolote zaidi ya kusubiri taarifa rasmi kutoka Caf,” alisema Kidao.

Nchi nyingine inayotishia nafasi ya Tanzania kuingiza timu nne katika mashindano ya klabu Afrika msimu ujao ni Ivory Coast yenye pointi tisa ambayo inaweza kuongeza pointi zake ikiwa klabu yake ya RC Abidjan itafikia mbali katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kenya na Zimbabwe ambazo timu zao za Gor Mahia na FC Platinum zitacheza hatua ya mwisho ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika nazo ni tishio lingine kwa Tanzania kwani kila moja ina pointi nane na zinaweza kuongezeka ikiwa zitafanya vizuri na kumaliza katika nafasi za juu zaidi katika mashindano hayo.

Ukiondoa hizo, pia kuna Senegal kwani yenyewe ina timu ya Teungueth iliyopo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ina pointi nyingi zaidi ya zile za Kombe la Shirikisho Afrika. Senegal yenyewe hadi sasa imekusanya pointi tano.

Mwanaspoti

No comments: