Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Wananchi 27 waliojimilikisha bila uhalali ekari 12,000 ya maeneo ya ardhi ya Kijiji cha Emboreet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamenyang’anywa ardhi hiyo na kurejeshwa mikononi mwa Serikali ya Kijiji hicho.
Wananchi hao 27 walijimilisha ekari 1,000 na wengine ekari 500 tangu mwaka 1993 bila kuwa na nyaraka zozote zinazowaruhusu kumiliki.
Kamishina msaidizi wa ardhi wa mkoa wa Manyara, Leonard Msafiri ametoa uamuzi huo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Emboreet.
Msafiri amesema endapo wananchi hao bado wanahitaji ardhi hiyo wawasilishe maombi na yajadiliwe upya na taratibu zifuatwe.
Amesema eneo hilo lilitengwa katika mpango wa matumizi ya ardhi ya Emboreet ambapo matumizi hayakinzani na masuala ya hifadhi ya wanyama pori.
Amesema ardhi hiyo inabaki kwenye serikali ya kijiji kwa ajili ya matumizi yaliyoainishwa kwenye mpango wa miaka 10 wa matumizi ya kijiji hicho cha Emboreet.
“Katika mgogoro huu unaweza kujiuliza je waliopewa ardhi na wanamiliki kwa nyaraka gani? je kuna upimaji uliofanyika? je ramani za kipabde cha kila moja kipo? amehoji Msafiri.
Mkazi wa kijiji cha Emboreet, Raymond Kosyando amesema wananchi hao walijimilikisha ardhi hiyo bila kushirikisha wana kijiji ambao ndiyo wenye mamlaka ya kugawa ardhi.
“Hatuna shida na wananchi hao ila wanapaswa kutambua kuwa walipata maeneo hayo bila kuwa na nyaraka zinazowaruhusu kumiliki ardhi hiyo,” amesema Kosyando.
Diwani wa kata ya Emboreet, Yohana Shinini amempongeza Msafiri kwa kutatua mgogoro huo wa miaka mingi ambao umezorotesha shughuli za maendeleo za eneo hilo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho amewataka wananchi wa eneo hilo kutoshangilia uamuzi huo kwani hakuna upande ulioshinda na pia wote ni jamii moja hivyo waendeleze upendo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake