Tuesday, August 31, 2021

WAZIRI JAFO ATOA MIEZI SITA KWA MAKAMPUNI YA MOTISON GROUP KUTENGA ENEO LA KUHIFADHIA BIDHAA ZA VINYWAJI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani jafo akikagua mfereji wa maji yaliyotibiwa kwenye kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola kwanza Jijini Dar Es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani jafo akitoa maelekezo kwa viongozi wa kiwanda cha Iron & Steel kuhusu kufunga mtambo maalumu wa kuzuia moshi kuzagaa kwenye mazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo ametoa miezi sita kwa wamiliki wa kiwanda Cha Sayona kinachomilikiwa na Kampuni ya Motison Group ambacho kinazalisha bidhaa za plastiki, rangi na Chuma kuhakikisha kinatenga eneo maalumu la kuhifadhia bidhaa za vinywaji ili kuepuka kuchanganyika na bidhaa zisizo za chakula zinazo zalishwa kiwandani hapo.

Ameyasema hayo alipofanya ziara kwenye kampuni ya Motison Group inayomilikiwa na kampuni ya Sayona, Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

“Kiwanda hiki mmejitahidi kwenye mfumo wa kutibu maji, lakini tatizo nililolibaini ni kwamba mnaweka bidhaa za vinywaji sehemu moja na bidhaa nyingine kama rangi na plastiki jambo ambalo ni hatari kwa afya zetu. Ninatoa miezi sita kuanzia sasa mtenge sehemu maalumu ya kuhifadhia bidhaa za vinywaji ili kuepuka madhara ya kiafya ya mtumiaji wa vinywaji mnavyozalisha hapa.”

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amekataa kusaini kibali cha kukusanya chuma chakavu kwenye kiwanda cha Iron & Steel kilichopo Mikocheni Jijini Dar es salaam mpaka kitakapoweka mfumo mzuri wa kuzuia moshi usisambae angani. Waziri Jafo amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi walio karibu na kiwanda hicho kutoa moshi unaoleta athari kwa afya zao.

” Viwanda vinatoa ajira kwa Wananchi wetu, mbali na hilo vinalipa kodi kwa Serikali yetu. Pamoja na hizi faida ni lazima tuzingatie utunzaji wa mazingira yetu. Kiwanda hiki hakina mfumo mzuri wa kutoa moshi jambo ambalo ni hatari kwa afya ya wakazi wa eneo hili, hivyo naagiza wafanye marekebisho ili wapate kibali cha ukusanyaji wa vyuma chakavu.” amesema Waziri Jafo.

Aidha Waziri Jafo amekipongeza kiwanda cha Coca-cola kwanza kilichopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam kwa jitihada na harakati za utunzaji wa Mazingira. Amewapongeza kwa kuunda mabalozi wa Coca-cola wanaokusanya chupa za plastiki kwa ajili ya kurejelezwa (recycling).

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake