Thursday, September 2, 2021

KATIBU TSC ASIKITISHWA NA WALIMU WANAOHITIMISHA UTUMISHI KWA KUFUKUZWA KAZI

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama akijibu hoja mbalimbali za walimu waliohudhuria kongamano la walimu wenye ulemavu kutoka Wilaya za Tanzania Bara lililofanyika hivi karibuni jijini Dodoma. Kongamano hilo liliandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka TSC, Wakili Richard Odongo akiwasilisha mada kuhusu Sheria na Kanuni za Utumishi wa Walimu katika kongamano la walimu wenye ulemavu Tanzania Bara lililofanyika hivi karibuni jijini Dodoma. Kongamano hilo liliandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Christina Hape akiwasilisha mada kuhusu Historia ya TSC pamoja na Nguzo za Maadili ya Kazi ya Ualimu katika kongamano la walimu wenye ulemavu Tanzania Bara lililofanyika hivi karibuni jijini Dodoma. Kongamano hilo liliandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka TSC, Moses Chitama akiwasilisha mada kuhusu Muundo wa Tume hiyo katika kongamano la walimu wenye ulemavu Tanzania Bara lililofanyika hivi karibuni jijini Dodoma. Kongamano hilo liliandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Walimu wenye mahitaji maalum wakifuatilia mada kuhusu masuala ya TSC kupitia mkalimani wa lugha ya alama.
Mwalimu Hellen Mbando kutoka Kilimajaro akiuliza swali mara baada ya viongozi kutoka TSC kuwasilisha mada wakati wa kongamano la walimu wenye ulemavu Tanzania Bara lililofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.

Na Adili Mhina.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama amesema anaumizwa na walimu kuhitimisha utumishi wao kwa kufukuzwa kazi kutokana na kuwa na tabia zinazokwenda kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu.

Nkwama ameyasema hayo wakati akijibu maswali yaliyoulizwa na walimu kuhusu taratibu mbalimbali za utumishi wa walimu katika kongamano la walimu wenye ulemavu Tanzania Bara lililoandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Katika kongamano hilo lililofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, Nkwama alieleza kuwa Serikali inapomwajiri mwalimu inatarajia mtumishi huyo adumu katika utumishi wake hadi pale atakapotimiza umri kustaafu kwa mujibu wa sheria au kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa mwanadamu.

“Mara nyingi mwalimu anaajiriwa akiwa kijana na sisi tunatarajia kuwa atadumu katika utumishi wa umma na kufaidi haki zake zote hadi umri wake wa kustaafu utakapofika. Lakini kwa kweli inasikitisha sana pale ambapo unakuta mwalimu anaajiriwa lakini baada ya muda anafukuzwa kazi na wakati huo kuna watu nyuma yake ambao kuishi kwao kunategemea ajira yake,” alisema Nkwama.

Alifafanua kuwa TSC imejikita katika kuwaelimisha walimu juu ya taratibu za utumishi wao ili watekeleze majukumu yao bila kuvunja taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2016.

Aliendelea kueleza kuwa pamoja na kupungua kwa mashauri ya nidhamu kutokana na jitihada za kutoa elimu, bado kuna walimu wachache ambao wanaojihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na Miiko na Maadili ya kazi ya ualimu na kujikuta wakikatisha ajira zao kwa kufukuzwa kazi.

“Tumefanya jitihada mbalimbali za kutumia kila fursa inayopatikana kwa ajili ya kuwaelimisha walimu, tunashukuru kuona kwamba kuna mabadiliko. Lakini sisi lengo letu ni kuona kila mwalimu anazingatia yale aliyoelekezwa, tunaumia tukiona bado kuna walimu wanaofukuzwa kazi,” alisema Katibu wa TSC.

Katibu huyo alisisitiza kuwa pale TSC inapoendesha shauri la nidhamu la mtu inahakikisha inasimama katika haki kwa mujibu wa sheria bila kupendelea au kumuonea mtu, na pale inapotokea kuna upande usioridhika na uamuzi kuna haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa sheria.

“Hapa tunashauriana na kuelimishana ili tuzingatie sheria kwenye utendaji wetu wa kazi lakini linapokuja shauri la nidhamu, hapo hakuna muda wa mjadala tena tunachoangalia ni sheria peke yake, kama mwalimu atakutwa na hatia ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria na kama hajapatikana na hatia ataachiwa huru,” alieleza Nkwama.

Akiongelea suala la haki kwa mtuhumiwa wa shauri la nidhamu, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoa TSC, Wakili Richard Odongo alieleza kuwa mtuhumiwa ana haki ya kupewa hati ya mashtaka inayoeleza kosa, wakati na namna kosa lilivyofanyika.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa lazima apewe muda wa kutosha kujitetea na endapo hatawasilisha utetezi, utetezi aliowasilisha haujitoshelezi au amekanusha tuhuma ni lazima iundwe kamati ya uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza shauri hilo. Odongo alieleza sifa za wajumbe wa kamati ya uchunguzi kuwa lazima wawe watumishi wa umma, wawe wamefikia cheo cha uandamizi au zaidi, wawe na cheo kikubwa zaidi ya anayechunguzwa na kamati hiyo inatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua wawili na wasiozidi wanne huku ikisisitizwa kuzingatia jinsi.

Wakili huyo alihitimisha mada yake kwa kueleza haki za mwalimu anayechunguzwa kuwa ni kujulishwa muda, siku, mahali na tarehe ambapo uchunguzi wa shauri lake utafanyika, kuwepo au kuwa na uwakilishi wakati wa uchunguzi wa shauri lake, kuhoji mashahidi na kupewa kielelezo chochote kinachotumiwa kama ushahidi dhidi yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Christina Hape, alieleza kuwa tangu Tanzania ipate uhuru walimu wamekuwa na chombo cha kushughulikia utumishi wao ikiwa ni juhudi za serikali kutambua umuhimu wa kundi hilo.

Alieleza kuwa walimu wana kazi kubwa kwani wao ndio wenye jukumu la kutengeneza watu wenye uwezo wa kufikia malengo ya Taifa kwa kuwa wanaanza kumjenga mwanafunzi tangu akiwa mtoto hadi anapokuwa mtu mzima, amesisitiza walimu kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa weledi ili Tanzania iendelee kupiga hatua zaidi katika maendeleo.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka TSC, Moses Chitama aliwaeleza washiriki hao muundo wa Tume hiyo kuwa unahusisha Mwenyekiti, Katibu, Wajumbe pamoja na Idara mbili na Vitengo saba vilivyoko ndani ya Tume.

Kwa upande wa Ofisi za Tume ngazi ya Wilaya, Chitama alieleza kuwa Masula ya Walimu yanaamuliwa na Kamati ya Wilaya ambayo inaundwa na wajumbe mbalimbali huku Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya akiwa ndiye Katibu wa Kamati ya Wilaya na mtendaji mkuu wa Tume kwa ngazi ya Wilaya.

2 comments:

  1. Naomba usaidizi wakaro ili niweze kuunga na chuo kikuu

    ReplyDelete
  2. Hello Niko nashida ya karo

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake