Madereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Mlowo na Tunduma mkoani Songwe wamesitisha huduma za usafirishaji wa abiria wakidai wanasubiri tamko la Serikali la kupandisha nauli.
Madereva hao wamesiitisha huduma jana Jumanne Aprili 19, 2022 huku wananchi wakiteseka kutafuta njia mbadala kufika maeneo mbalimbali.
Baadhi ya abiria wamelazimika kutumia usafiri wa bajaji na bodaboda kufika kwenye maeneo wanakofanya shughuli zao.
Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva wa Haice za Tunduma na Mlowo, Fadhili Bernad amesema wameanza mgomo huo baada ya kuona ukimya wa Serikali kutotoa tamko lolote juu ya bei elekezi ya nauli za daladala kutokana na ongezeko la bei za mafuta ya dieseli na petroli.
Bernad amesema kwa sasa wanalazimishwa kutumia bei ya awali ambayo ni Sh500 kila kituo badala ya 1000 jambo ambalo wamesema haliwapi faida yoyote kutokana na ongezeko la mafuta.
Mwananchi limeshuhudia umati wa abiria katika kituo cha daladala cha Mpemba waliokwama kuendelea na safari kwenda Tunduma.
Mmoja wa abiria hao, Edward Kalinga wamewasihi madereva kuacha mgomo badala yake amewashauri kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kuandaa bei elekezi.
Meneja wa Latra Mkoa wa Songwe, Joseph Burongo amesema hana taarifa yoyote kuhusiana na mgomo huo na kwamba atafuatilia na atatoa majibu baadaye.

No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake