ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 14, 2022

MWENDO KASI MAMBO MAZURI YAJA TEGETA, KAWE


WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), itaendelea kukamilisha usanifu, ambapo awamu ya nne itahusu barabara za Bibi Titi, Alli Hassan Mwinyi na Bagamoyo hadi Tegeta pamoja na Barabara ya Sam Nujoma.

Hayo yamesemwa leo Aprili 14, 2022, bungeni Dodoma na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo.

Amesema awamu ya tano itajumuisha Barabara za Nelson Mandela kuanzia Ubungo hadi Daraja la Mwalimu Nyerere-Kigamboni, Tabata na Kigogo kuanzia Tabata Segerea kupitia Tabata Dampo, Kigogo hadi Barabara ya Kawawa zenye urefu wa kilomita 27.6.

Amesema usanifu wa awamu ya sita utajumuisha barabara ya Mwai Kibaki hadi Kawe, nyongeza ya barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kibamba na barabara ya Kilwa kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Vikindu yenye urefu wa kilomita 26.5.

Amesema mwaka wa fedha 2022/23, Wakala wa Mabasi yaendayo haraka, ataendelea na uboreshaji wa huduma za usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) mkoani Dar es Salaam na maeneo ya jirani, ikiwa ni pamoja na kuendelea na usimamizi wa utoaji wa huduma ya usafiri wa haraka.

“Tutakamilisha taratibu za manunuzi ya mtoa huduma wa mabasi 95 ya nyongeza kwenye awamu ya kwanza ya BRT na kubadilisha mfumo wa uendeshaji na ulipaji wa watoa huduma kutoka kupokea tozo ya kupita katika mfumo wa DART na kuanza kutumia utaratibu wa malipo ya umbali, ambao mabasi yatakuwa yanatembea,” amesema Bashungwa

No comments: