ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 10, 2022

JAFO ASITISHA UINGIZAJI WA NGOZI KATIKA GHALA LA KUHIFADHI NGOZI KURASINI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea ghala la kuhifadhi ngozi ghafi lililopo Kurasini Temeke jijini Dar es Salaam tarehe 09 Mei 2022.
Mwekezaji wa Kiwanda cha kurejeleza chupa za plastiki cha A – One kilichopo Mbagala – Temeke jijini Dar es salaam Bw. Prashant Plaint akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo kutembelea kiwanda hicho Mei 09,2022.
Baadhi ya ngozi ghafi zikiwa zimehifadhiwa katika ghala maalumu kabla hazijaanza kutumika katika shughuli mbalimbali
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiambata na baadhi ya watumishi wa NEMC wakiwasili katika ghala la kuhifadhi ngozi ghafi lililopo Kurasini Temeke jijini Dar es salaam tarehe 09 Mei 2022.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo amefanya ziara ya kukagua mazingira katika ghala la kuhifadhi ngozi ghafi lililopo Kurasini Temeke jijini Dar es salaam tarehe 09 Mei 2022.

Ukaguzi huo umefanyika baada ya kupokea malalamiko ya harufu mbaya kutoka kwa wakazi wanaoishi karibu na ghala hilo.

Waziri Jafo amesema Wizara yake imepokea malalamiko kuwa kuna ghala linalohifadhi ngozi ghafi karibu na makazi ya watu na kusababisha kusambaa kwa harufu kali kwenye makazi ya watu na hata watu kushindwa kukaa ndani ya nyumba zao.

Hata hivyo taarifa hizo zilishafika kwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na wameanza kuchukua hatua ili kuondokana na adha hiyo kwa wakazi wa eneo hilo.

Aidha Waziri Jafo amesema baada ya kupokea malalamiko hayo Wizara yake imetoa agizo la kusitisha uingizaji wa ngozi nyingine katika ghala hiyo na kutoa ushauri kwa msimamizi wa ghala hilo Bw. Shiri Mwandu,

” Eneo kama hili lingeweza kuhifadhiwa bidhaa zingine kama mbao, saruji, nondo na bidhaa zingine ambazo zingeweza kuwa rafiki kwa mazingira haya, kwa sababu eneo hili lipo ndani ya makazi ya watu ili kuepuka changamoto za uharibifu na uchafuzi wa mazingira. sambamba na hilo fanyeni utaratibu wa kupata cheti cha mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili tuweze kujiridhisha kama eneo hili linafaa kwa shughuli hii ya ngozi na kupata maelekezo ya utunzaji wa mazingira”. Amesema Waziri Jafo

Baada ya kutembelea ghala hilo pia Mhe. Jafo ametembelea kiwanda cha kurejeleza chupa za plastiki cha A – One kilichopo Mbagala – Temeke jijini Dar es salaam katika kukagua na kuona jinsi kiwanda hicho kinavyochakata na kurejeleza chupa hizo .

Waziri Jafo amesema kuwa amefurahishwa sana na kuanzishwa kwa kiwanda hicho ambacho kinarejeleza chupa za plastiki za aina zote hata za rangi ambazo hapo awali zilikuwa hazirejelezwi na zilikuwa zinazagaa hovyo mitaani na kuchafua mazingira .

“Nimefurahishwa sana kuanzishwa kwa kiwanda hiki na leo nimefika ili kuona jinsi kinavyofanya kazi na nimefurahishwa sana, niwaombe muongeze vituo vya ukusanyaji wa chupa hizi katika Mikoa yote Tanzania ili ziletwe katika kiwanda hiki na kurejelezwa, sitaki kuona chupa hizi zikizagaa hovyo mitaani.” Amesema

Kwa upande wake mwekezaji wa kiwanda hicho Bw. Prashant Plaint amesema anampango wa kuongeza nguvu zaidi katika uzalishaji na kwa mwaka ujao 2023 anatarajia kurejeleza chupa mara mbili zaidi ya sasa.

Naye Afisa Afya na usalama katika kiwanda hicho Bw. Aurus George amesema hii ni fursa kwa watanzania wale watakaokuwa wanakusanya chupa hizo na kuziuza kwao na pia watasaidia mazingira kuwa safi kwa kuwa kiwanda chao kinapokea chupa aina zote za rangi na chupa nyingine za kawaida.

Naye Afisa Tarafa ya Temeke Bi. Bertha Manga aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Temeke Mhe. Jokate Mwegelo ameshukuru sana ujio wa Mhe. Jafo kiwandani hapo na kusema wamepokea maelekezo yake na watatoa elimu zaidi kwa wananchi kukusanya chupa zote za plastiki bila kujali rangi za chupa hizo kwa kuwa sasa wataweza kuziuza kiwandani hapo.

No comments: