Advertisements

Sunday, June 11, 2023

DK.MWINYI AKEMEA MAKUNDI,ASEMA HAKUNA WA KUZUIA KASI YA CCM


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi,amewataka Wanachama wa Chama hicho kuweka kando dhana za makundi na badala yake waelekeze nguvu zao katika kujipanga na Uchaguzi Mkuu ujao wa Dola wa mwaka 2025.

Kauli hiyo aliitoa wakati akihitimisha ziara yake ya Kichama kwa upande wa Unguja huko katika Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda,alisema uwepo wa makundi ya wagombea ni kawaida ndani ya michakato ya kisiasa wakati wa Uchaguzi lakini makundi hayo yanatakiwa kuisha mara baada ya kuisha Uchaguzi na kupatikana Viongozi.

Dk.Mwinyi, alisema kuwa nguvu za CCM zinatokana na Umoja na Mshikamano wa Wanachama,Viongozi na Watendaji wa Chama hicho.

"Wanachama wenzangu naomba tuendelee kushikamana zaidi kwa maslahi ya Chama chetu,tusivurugwe na kuendekeza makundi ya wakati wa Uchaguzi,tayari Viongozi wamepatikana na uchaguzi wa Chama umekwisha na sasa tujielekeze katika Uchaguzi wa Dola 2025.",alisema kwamba.

Alisema kwamba katika michakato ya Kidemokrasia ukisikia adui anakusifia ujue kuna tatizo na ukimsikia mpinzani anakushambulia ujue umemshika ndipo.

Alifafanua kwamba wapinzani wa nchini kwa sasa hawana akenda kutokana na utekelezaji wa Ilani,na kwa sasa wametengeneza vibaraka naopotosha na kuhoji ushindi wa CCM vitendo vinavyotakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Alielekeza Kamati za Maadili za CCM,kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na kuacha utamaduni wa kusubiri wakati wa Uchaguzi ndio wachukue hatua kwa wanaokiuka Maadili ya Chama.

"Kuna watu wameanza kuwa vibaraka wa wapinzani kwa kupotosha na kutoa kauli zisizofaa kwa Wanachama na Wananchi kama mtu hakitaki Chama aondoke tu lakini asituharibie Chama Chetu",alisisitiza Dk.Mwinyi.

Katika maelezo yake Dk.Mwinyi,alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Viongozi na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kumuamini na kumchahua kwa kura nyingi kushika nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti.

Alisema nguvu za CCM zinatokana na Umoja na Mshikamano imara unaojengwa na Wanachama wote wa CCM na Jumuiya zake.

Alisema dhamira ya Serikali ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa Kasi kubwa na kwa viwango ambapo kwa sasa zaidi asilimia 100 ya utekelezaji wa Ilani imekamilika.

Alisema katika ukanda wa Kaskazini Unguja,Bandari ya Mwangapwani ndio kubwa na itakayosaidia kuchochea ukuaji wa Uchumi nchini.

Alisema katika kumaliza tatizo la upungufu wa tatizo la maji katika Mkoa huo Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa na kwamba tatizo hilo litaondoka hivi karibuni.

Alisema CCM imejipanga kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo yake ili iweze kuwa na miradi yake yenyewe itakayozaliza rasilimali fedha na kujitegemea kiuchumi.

Aliwataka Viongozi wa Mkoa huo kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuingiza Wanachama wapya na kuhimiza ulipaji wa ada.

Pamoja na hayo alisema,Chama kitaendelea kuthamini juhudi za Mabalozi wa mashina kwa mchango wao katika kusimamia maslahi ya CCM.

Dkt.Dimwa, alisema Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi,ameendelea kutekeleza kwa kasi kubwa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa kuhakikisha Wananchi wananufaika na fursa za maendeleo Mijini na Vijijini.

Alisema Serikali tayari imekamilisha ujenzi wa Madarasa 158 na zinaendelea kujengwa skuli tano za ghorofa za kisasa ndani ya Mkoa huo ili kuimarisha sekta ya Elimu.

Alieleza kuwa CCM itaendelea kuzisimamia na kuzielekeza Serikali ili iendelee kutoa huduma bora na zenye viwango kwa jamii.

"CCM ndio Chama pekee chenye kuleta Mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo kwa Wananchi wote wa Visiwa vya Zanzibar,hivyo tuendelee kuunga mkono",alisema Dkt.Dimwa.

Kwa upande wake,Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,alisema ndani ya Mkoa huo kinajengwa kiwanda cha kusindika Samaki ili kuongeza thamani ya Samaki na mazao ya Bahari.

Alisema kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi ZIPA) jumla ya miradi 230 imesajiliwa asilimia 60 ya miradi hiyo inatekelezwa Kaskazini Unguja kwa lengo la kuongeza fursa za uwekezaji.

Alisema Serikali ina mkakati wa kujenga Skuli kubwa ya kisasa ya daharia katika maeneo ya katika Mkoa huo ili kutoa fursa pana kwa wanafunzi kupata elimu katika mazingira rafiki na salama.

Akizungumza Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,Ayoub Mahmoud Mohamed,akitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa kazi za Serikali ndani ya Mkoa huo alisema hali ya amani na Usalama ipo shwari.

Amesema Wananchi wanampongeza Kwa Kasi yake ya utendaji kwani ndani ya Mkoa huo amefanya mengi makubwa na kujivunia katika nyanja za kisiasa,kiuchumi na kijamii.

Alisema katika Sekta ya Afya wapo katika hatua za mwisho kukamilisha hospitali ya Mkoa ili kutoa huduma bora za Afya.

Katika upande wa sekta ya miundo mbinu jumla ya km 32 za barabara za lami zimekamilika na zingine zinajengwa.

Kwa upande wa sekta ya maji tayari vinajengwa matangi mawili makubwa.

Alisema dhamira ya Dk.Mwinyi,inafungua fursa kubwa za kiuchumi kupitia Bandari ya Mwanga pwani na maeneo mengi ya Uwekezaji.

Alisema kwamba katika sekta ya anga tayari Uwanja wa Ndege wa Nungwi utafanywa wa Kimataifa Kwa ajili ya kusafirisha watalii na Wananchi watakaokuwa na mahitaji ya usafiri.

Alifafanua kuwa katika Sekta ya Uchumi wa buluu alisema zaidi ya boti 200 zimetolewa kwa vikundi 27 vimekabidhiwa boti za uvuvi ili kwenda na mahitaji halisi ya dhana ya Uchumi wa buluu kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujiajiri kupitia Sekta ya Bahari.

Naye Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Dkt.Khalid Salum Mohamed,alisema Dk.Mwinyi,ameendelea kutekeleza Ilani kwa ufanisi katika eneo la miundombinu kwa kuendelea kujenga barabara za viwango vya lami katika Mkoa huo.

Alisema Mkoa huo una zaidi ya mtandao wa barabara wenye urefu wa zaidi ya Km 45.2 ambazo nyingi zina viwango vya lami.

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani Waziri wa Ustawi wa jamii,Jinsia Wanawake,Wazee na watoto Mhe.Riziki Pembe Juma, alimpongeza Dk.Mwinyi kwa kuongeza pensheni ya Wazee kutoka 20,000/= hadi 50,000/= kwa mwezi.

Alisema kwa sasa vikundi mbalimbali vya wanawake na makundi mengine wameendelea kupata mikopo na wamejenga jengo la kisasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya Ujasiriamali kwa wanawake

No comments: