Sunday, March 31, 2024

MAKAMU WA RAIS DKT MPANGO AUNGANA NA WAUMINI WENGINE WA KIKRISTO KWENYE IBADA YA SIKUKUU YA PASAKA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango leo tarehe 31 Machi 2024 wameungana na waumini mbalimbali kushiriki Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Yesu – Kisasa Mkoani Dodoma.
Akitoa salamu za Sikukuu ya Pasaka mara baada ya kushiriki Ibada hiyo, Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania kutumia sikukuu ya Pasaka kutambua hakuna ushindi bila kujitoa muhanga kwaajili ya wengine, familia, wahitaji na Taifa kwa ujumla.
Amesema ni lazima kujitoa muhanga kwa kutimiza wajibu vizuri kwa kufanya kazi kwa bidii kwaajili ya maendeleo ya nchi ya sasa na vizazi vijavyo. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kutumia sikukuu ya Pasaka kujifunza kushinda ubinafsi na kuhakikisha haki na huduma zinatolewa bila kuomba rushwa.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi na watumishi wa serikali kuwa kielelezo cha kujitoa muhanga kwaajili ya kuwatumikia watu wengine. Amesema watanzania wanapaswa kuendelea kumcha Mungu pamoja na kutunza urithi wa dunia uliyotolewa na Mwenyezi Mungu ikiwemo Mazingira
Ibada hiyo imeongozwa na Padre Vedastus Ngowi kwa kushirikiana na Paroko wa Parokia hiyo Sostenes Ndendya.








No comments: