Sunday, March 31, 2024

MWALIMU JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA


Na Hamisi Nasri MASASI

MAHAKAMA ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela Nestory Michael (23) mkazi wa wilaya ya Masasi ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Mkalapa iliyopo halmashauri ya wilaya ya Masasi kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wake mwenye umri miaka 13 (Jina linahifadhiwa) anayesoma darasa la saba katika hiyo ya msingi Mkalapa.

Akisoma hukumu hiyo jana mahakamani hapo hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo ya wilaya ya Masasi, Batista Kashusha alieleza kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa jamuhuri ambao umethibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa Michael pasipo shaka yoyote.

Hakimu Kashusha alidai mahakamani hapo kwamba wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo ambalo ni kesi namba 16 / 89 ya mwaka 2023 , upande wa jamhuri ulikuwa na mashahidi saba na kielelezo.

Alieleza kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri na mahakama kujiridhisha na ushahidi huo mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kosa hilo la ubakaji Kwa kifungo cha miaka 30 jela.

" Namtia hatiani mshtakiwa katika shitaka hili la ubakaji baada ya upande wa jamhuri kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa kwa kuleta mashahidi na vielelezo ikiwemo kielelezo cha daktari hivyo ninamuhukumu kifungo cha miaka 30 jela," alisema hakimu kashusha

Hakimu Batista alidai kuwa hukumu hiyo imezingatia mambo yote ya msingi ya kisheria ikiwa ni pamoja na kubaini kuwa kweli tukio la ubakaji limetokea Kwa kujiridhisha na vielelezo vya ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri.

Awali, mkuu wa mashtaka wilaya ya Masasi ambaye ni wakili wa serikali mwandamizi ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali( DPP) wilaya ya Masasi, Miraji Kajieul aliiomba mahakama kuwa itowe adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na kosa alilotenda.

Wakili huyo wa upande wa serikali alidai kuwa iwapo mahakama itatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa Ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kufanya vitendo kama hivyo vya ubakaji.

Wakili Kajieul alieleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 26 mwaka 2023 katika maeneo ya shule hiyo ya Mkalapa majira ya mchana.

Mshtakiwa aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu kwa kuwa yeye ni baba wa familia ya watoto wawili na mke mmoja na mama yake mzazi ambapo wote kwa pamoja wanamtegemea kimaisha.

No comments: