Advertisements

Sunday, April 14, 2024

WAZIRI MASAUNI AWAJULIA HALI ASKARI ZIMAMOTO WALIOJERUHIWA KWA MOTO WAKIFANYA UOKOAJI


WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amewajulia hali askari wawili wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji waliojeruhiwa wakati wa harakati za kuokoa majeruhi waliokuwa kwenye magari matatu yaliyowaka moto baada ajali kutokea eneo la Mlandizi mkoani Pwani.

Askari hao waliojuliwa hali na Waziri Masauni ni 3463 Koplo Hamisi Kungwi ambaye yupo Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na 3384 Koplo Elias Bwire yupo wodi ya kawaida, wote wapo katika Hospitali Taifa ya Muhimbili Mloganzila jijini Dar es Salaam wakiendelea kupatiwa matibabu.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akimpa pole ,Elias Bwire

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Aprili 12,2024 baada ya kuwajulia hali askari hao, Waziri Masauni amesema amekuwa taarifa za askari hao kwa muda wote wanaoendelea kupatiwa matibabu na leo amefika kuwajulia hali.

"Nimekuja nakujionea mwenyewe jinsi ambavyo afya za askari hawa zinavyoendelea kuimarika, kiukweli huduma na mazingira ya hospitali ni mazuri.Tunazidi kuwaombea ili afya zao ziendelee kuwa nzuri na hatimaye warudi nyumbani kuungana na familia zao."

Aidha amesema Serikali inaendelea kuliangalia eneo la uwekeza katika mafunzo ili kuwasaidia askari wanapotekeleza majukumu yao wawe na uelewa mkubwa zaidi.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, Dk. Julieth Magandi amesema askari hao wanaendelea vizuri na matibabu katika hospitali hiyo.

Amesema kuwa wao madaktari wanatibu lakini Mwenyezi Mungu anaponya na hivyo wanaendelea kuwaombea ili wapate nafuu ya haraka na afya njema na hatimaye wapone na watoke hospitali waendelee na majukumu yao ya kawaida.

Awali askari ambaye amèlazwa hospitali hapo, Koplo Bwire amesema anamshukuru Waziri Masauni pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuwajulia hali na kuwapa mkono wa pole baada ya kupatwa na changamoto hiyo.

No comments: