Advertisements

Friday, June 28, 2024

JESHI LA POLISI LAOMBA USHIRIKIANO KUTOKOMEZA UKATILI WA WATOTO SONGWE


Na Baraka Messa, Songwe.

KTOKANA na matukio ya ukatili kwa watoto chini ya miaka 8 kuendelea kutokea mara kwa mara mkoani Songwe jeshi la polisi limewataka wananchi kutoa taarifa za ukatili kwa Jeshi la Polisi ili watuhumiwa wawe wanafikishwa kwenye vyombo vya dola na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe Kamshna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga amesema pamoja na jeshi la polisi kutoa elimu ya mara kwa mara, lakini bado wanahitaji ushirikiano wa karibu kudhibiti matukio ya ukatili kwa watoto chini ya miaka nane ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara hivi karibuni.
Anasema tabia ya kumaliza kesi za ukatili kifamilia inasababisha matukio hayo kuongezeka katika mkoa wa Songwe na kuhatarisha jamii kupoteza nguvu kazi kwa miaka ijayo.

"Njia sahihi ya kukabiliana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea kutokea katika mkoa wa songwe ni jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za waharifu kwa viongozi waliokaribu nao ili taarifa hizo kufikishwa katika vituo vya Polisi kwa ajili ya hatua kali za kisheria dhidi yao , ambapo jamii itajifunza na kuogopa kufanya vitendo hivyo" anasema Kamanda Senga.

Anaeleza kuwa vitendo vya ukatili ambavyo hufanyiwa watoto na jamii kuvifumbia macho kwa kuwaficha waharifu kuwa ni pamoja na ulawiti, ubakaji , vipigo na mimba za utotoni.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Nambizo wilayani Mbozi katika ziara ya kutoa elimu kuhusiana matukio ya ukatili amewasisitiza wananchi pindi wafikishapo taarifa hizo katika vituo vya Polisi wahakikishe wanafuatilia kwa karibu kesi zao ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano mahakamani ili watuhumiwa hao waweze kupata adhabu kwa mujibu wa sheria kwa lengo la kutokomeza vitendo vibaya vinavyokwamisha ndoto za watoto katika Mkoa wa Songwe.

"Hivi karibuni Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe tumefanikiwa kuwashikilia wanaume wawili (02) ambao ni, wakazi wa Kaloleni Wilaya ya Songwe wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini kwa tuhuma za kumbaka na kumuua mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili na nusu, mkazi wa kaloleni" anasema

Pia katika mwezi mei anasema wamefanikiwa kumfikisha mahakamani Saimon Mwakasula (30) kwa kosa la kubaka katika mahakama ya wilaya ya Momba, mwingine ni Yohana Lot 36 kwa kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi hivyo kuhukumiwa miaka 30 katika mahakama ya wilaya ya Mbozi.

Afisa elimu shule za msingi na awali wilaya ya Mbozi Dorothy Mwandila anasema ubize wa wazazi katika shughuli za kiuchumi kumekuwa na athari kubwa katika malezi ya watoto, kwani watoto wengi hulazimika kulelewa na watu wengine ambao sio wazazi na kupata madhara.

"Watoto wetu tuwalee wenyewe, tuache kuwategemea ndugu wengine na majirani kutulelea watoto wetu, kwa sababu matukio yaliyo mengi ya ulawiti na ubakaji kwa watoto chini ya miaka nane hufanywa na ndugu wa karibu" anasema Mwandila.

Anasema pamoja na umuhimu wa shughuli za kiuchumi wazazi wajitahidi kutenga muda wa kukaa karibu na watoto ili kuhakikisha wanapata malezi yenye upendo, usalama huku wakiwasaidia kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

"Kuna madhara makubwa ya kutokuwa karibu na watoto, kuna kisa kimoja watoto wa mama mmoja baba mmoja kaka yao alikuwa anawaingilia kinyume na maumbile wadogo zake wawili chini ya miaka 10 bila wazazi wao kujua kutokana na ubize wa kuondoka asubuhi na kurudi usiku nyumbani"

Baada ya mama yao kugundua ambapo ilikuwa ni baada ya muda mrefu kufanyiwa ukatili huo watoto walieleza kuwa walikuwa wanaogopa kusema kutoka na kaka yao kuwatishia kuwachinja ikiwa watasema " alieleza Mwandila.

Kwa upande wake David Songoro Mwenyekiti wa baraza la ushauri wilaya ya Mbozi anasema ni vema wazazi na walezi wajikite katika malezi yanayozingatia maadili, desturi na kuwa na hofu ya mwenyezi Mungu.

Naye George Kiwaya kutoka kata ya Vwawa anasema katika wilaya ya Mbozi kumekuwa na changamoto nyingi za malezi kutokana na baadhi ya nyumba za kuishi kugeuzwa kuwa vilabu vya pombe za kienyeji hivyo watoto kuiga tabia mbaya wanazoziona kwa wakubwa wao.

"Ni vizuri vilabu vya pombe viwe vinatengwa mbali na maeneo ya makazi ili kunusuru vizazi vya watoto wetu ambao wanaathirika zaidi pindi vilabu vinapokuwa katika maeneo ya makazi" amesema Kiwaya.

Programu jumuishi ya Taifa ya malezi makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) inasisitiza kuwekeza kwa mtoto mdogo akiwa chini ya miaka nane ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto walio katika mazingira hatarishi wanalindwa dhidi ya hatari za kimwili na kihisia ambazo zinawazunguka.

No comments: