Friday, June 21, 2024

MBUNGE LUGANGIRA AONGOZA MAANDAMANO KUPINGA UKATILI


WANAWAKE wa Mkoa wa Kagera wakiongozwa na Mbunge wa Viti Maalum mkoani hapo Neema Lugangira wamefanya maandamano kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, ikiwa ni siku chache baada kifo cha mtoto wenye Ualbino Asimwe Novatus miaka miwili na nusu kuuwawa wilayani Muleba.

Akizungumza baada ya kufika nyumbani kwa kina Asimwe na kumpa pole mama mzazi, Mbunge Lugangira amesema tukio hilo limemuumiza Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa ujumla na kwamba watahakikisha wahusika wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
"Tumefanya maandamano haya ya amani kupinga mauji ya kikatili kwa mtoto Asimwe, lakini pia kupinga mauji yoyote ya aina hii, kwani huo sio utaratibu wa maisha yetu, inasikitisha sana, tunawapa pole wafiwa wote hasa mama," amesema.

Amesema Rais Samia ameelekeza vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi mchana na usiku kuhakikisha wahusika wanakamatwa na hatua stahiki zichukuliwe.

Aidha, Mbunge Lugangira ameahidi waombolezaji kutafuta wadau na kuanzisha kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu kulinda wenzetu wenye ualbino, kukataa kutumika na kupinga vikali ukatili wa aina zote kwa albino.

Mbunge huyo aliambatana na Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mkoa Kagera, Mwenyekiti UWT Wilaya ya Muleba, Katibu UWT Wilaya ya Muleba, Madiwani Viti Maalum kutoka Wilaya ya Muleba na wanachama wa UWT na CCM.

No comments: