Tuesday, July 30, 2024

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR MHE.HEMED SULEIMAN AENDELEA NA ZIARA YAKE NA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO PEMBA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wananchi wa Mzambarau Takao mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa soko la samaki na mboga mboga linalijengwa katika eneo hilo akiwa katika ziara zake za kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa Kisiwani Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema hajarizishwa na maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Chake-Wete inayojengwa na Mkandarasi Kampuni ya MECCO iliyotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa nane mwaka huu lakini hadi sasa ujenzi huo bado Unasuasua.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara hiyo ambayo kutokukamilika kwake imekuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi wanaoitumia barabara hiyo kwa shuhuli mbali mbali za kujitafutia kipato.

Mhe. Makamu wa Pili wa Rais ameitaka Kampuni ya MECCO kujitathmini na kufanya uharaka wa kukamilisha ujenzi wa barabara hio ili kurejesha Imani kwa wananchi ambao wanapata usumbufu kutokana na uchakavu wa barabara hiyo na endapo watashindwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa watakuwa wamejinyima fursa ya kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa kumekuwa na ubabaifu wa hali ya juu kwa baadhi ya wakandarasi wanaojenga miradi ya Serikali kwa kutotimiza makubaliano ya mikataba jambao ambalo linaisababishia hasara kubwa Serikali kwa kutofikia malengo ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko la samaki na mboga mboga lililopo Mzambarau Takao na soko la wajasiri amali Kifumbikai Wete Makamu wa Pili wa Rais ametoa mwezi mmoja kwa wananchi waliokwisha kulipwa fidia kuondoka katika eneo hilo ili kupisha ujenzi wa soko pamoja na kupisha utanuzi wa Barabara.

Amesema kuendelea kuwepo kwa wananchi hao katika eneo hilo kunakwamisha maendeleo ya ujenzi huo ambao kukamilika kwake kutawaondolea wananchi wa Mzambarau Takao na vijiji jirani changamoto ya kufata huduma ya soko maeneo ya mbali pia litatoa fursa kwa wananchi kuweza kufanya biashara zao katika mazingira mazuri na salama.

Aidha Mhe. Hemed amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Kampuni mbali mbali zinazojenga miradi ya maendeleo Zanzibar ili kuhakikisha miradi hio inamalizika kwa wakati uliopangwa na kuwaondolea kero wananchi wa Unguja na Pemba.

Kwa upande wao Mawaziri wa Wizara zenye dhamana ya kusimamia miradi hio wamesema kuwa watahakikisha kwa hali yoyote ile miradi ambayo ipo chini wa wizara zao inamalizika kwa wakati uliopangwa ili kuendana na dhamira ya Rais Dkt Hussen Mwinyi ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Mawaziri hao wamewataka wakandarasi wa ujenzi wa miradi hio kuhakikisha wanaongeza nguvu kazi za kutosha sambamba na kuongeza kasi ya ujenzi ili kumaliza mradi hio kwa wakati kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi kwa ujumla.

Nao wakandarasi wanaojenga miradi hio wamesema ujio wa Mhe. Makamu wa Pili wa Rais utatatua changamoto mbali mbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa malipo jambo ambalo husababisha kuzorota kwa ujenzi wa miradi hiyo.

Hata hivyo wamemuahidi Mhe.Makamu wa Pili wa Rais kuwa watafanya kazi kwa jitihada zote ili kuhakikisha wanakamilisha miradi hio kwa wakati uliopangwa.

Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Mhe. Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ni Mradi wa Barabara ya Chakechake,Wete na Mradi wa Soko la Samaki na Mbogamboga Mzambarau Takao,Soko la Wajasiriamali kifumbikai, ujenzi wa kituo cha afya Jadida ,Ujenzi wa nyumba za Madaktari Kinyasini,kukagua m aendeleo ya Hospitali ya Wilaya Kinyasini,ujenzi wa Kituo cha Afya Kinyikani na ujenzi wa Kituo cha Afya Kiuyu Minungwini Wete Pemba.

Imetolewa na kitengo Cha Habari ( OMPR)

LEO tarehe 29.07.2024.

No comments: