Tuesday, July 30, 2024

WAZIRI MKUU AFUNGUA MKUTANO WA KITAIFA WA RASILIMALI WATU KATIKA SEKTA YA AFYA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Mpango Mkakati wa Nne wa Taasisi ya Benjamin Mkapa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Julai 30, 2024. Wengine kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Tasisi ya Mkapa, Helen Mkondaya, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mkapa, Dkt. Adeline Kimambo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya wa Zanzibar, kulia ni Nassor Ahmed Mazrui.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha nakakala za Mpango Mkakati wa Nne wa Taasisi ya Benjamin Mkapa baada la kuzindua mkakati huo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Julai 30, 2024. Wengine kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Tasisi ya Mkapa, Helen Mkondaya, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mkapa, Dkt. Adeline Kimambo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya wa Zanzibar, kulia ni Nassor Ahmed Mazrui.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Haspitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohamed Janabi aliyetoa maelezo kuhusu VIZA ya Matibabu katika maonesho yaliyoambatana na Ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Afya Sambamba na Kumbukumbu ya Hayati Benjamin Mkapa. Ufunguzi huo ulifanywa na Waziri Mkuu kwenye Kituo cha Mikutano cha Kijataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Julai 30, 2024. Wa pili kushoto ni Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui na wa tatu kushoto ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifuatilia matukio mbalimbali wakati alipowasili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam kufungua wa Mkutano wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Afya Sambamba na Kumbukumbu ya Hayati Benjamin Mkapa, Julai 30, 2024. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mkapa, Helen Mkondya na kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mkapa, Dkt. Adeline Kimambo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati lipofungua Mkutano wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Afya Sambamba na Kumbukumbu ya Hayati Benjamin Mkapa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Julai 30, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeimarisha nguvukazi kwenye sekta ya afya kwa kuongeza taasisi zinazotoa mafunzo ya afya na upatikanaji wa fursa za elimu ya juu kwa kada hiyo.

“Serikali imefanya upanuzi wa taasisi za mafunzo ya afya ili kuongeza idadi ya wahitimu. Taasisi hizo ni pamoja na vyuo vya uuguzi, ukunga na utabibu. Hivi sasa nchi yetu ina taasisi 182 zikiwemo taasisi 137 zinazomilikiwa na sekta binafsi. Ni jambo la faraja kuona kuwa katika mwaka 2023/2024 peke yake, vyuo hivyo vimedahili wanafunzi 40,000.”

Akizungumza na viongozi, wadau na watumishi walioshiriki ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Afya leo (Jumanne, Julai 30, 2024), Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita imehakikisha fursa za masomo ya elimu ya juu zinapatikana kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa.
“Lakini pia, wanafunzi wanaosomea kozi za afya wamekuwa wakipewa kipaumbele wakati wote kwa kupewa mikopo ya asilimia 100. Vilevile, suala la kuendeleza rasilimali watu limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kila mwaka ili kufanikisha ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi, stadi muhimu na wanaoweza kumudu mahitaji ya ndani na ushindani wa kimataifa,” amesema.

Akielezea kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali, Waziri Mkuu amesema Serikali imekwishaimarisha huduma ya afya ya msingi, huduma za afya katika ngazi ya wilaya na sasa inaimarisha huduma hizo kwenye ngazi ya Halmashauri.

“Tumeimarisha huduma za msingi, tumeimarisha hospitali za wilaya na sasa tunajenga hospitali za Halmashauri ili kupunguza umbali kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni. Sasa hivi tunaimarisha pia huduma za rufaa kama vile Benjamin Mkapa na Bugando,” amesema.

Akielezea kuhusu ajira na upangaji wa watumishi wa kada za afya, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, watumishi 30,000 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi vikiwemo vya vijijini. “Baadhi ya watumishi hao ni pamoja na madaktari, wauguzi pamoja na wakunga. Hii ni hatua kubwa sana ya maendeleo katika utoaji wa huduma za afya nchini,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa upatikanaji wa rasilmaliwatu, vifaa tiba na dawa vinaendelea kuwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo la siku mbili, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) imeandaa kongamano hilo kama sehemu ya kumkumbuka Hayati Rais Benjamin Mkapa lakini pia kutoa msisitizo wa haja ya kuendeleza rasilmaliwatu kwenye sekta ya afya.

Aliipongeza taasisi hiyo kwa kusimamia ndoto yao kuu ya kuzalisha watumishi kwenye sekta ya afya ambao kila wanapohitimu wamekuwa wanapangiwa ajira kwenye maeneo ya pembezoni kwa mkataba wa miaka mitatu. “Watumishi hawa wanafanya kazi nzuri sana huko waliko na wanapomaliza mkataba wao na taasisi hii, tumekuwa tunawachukua ili waendelee kutoa hudumakwa wananchi katika maeneo waliyoyazoea.”

Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Nassor Ahmed Mazrui alisema kwamba suala la uendelezaji wa rasilmaliwatu kwenye sekta ya afya ni la muhimu lakini akasisitiza haja ya kupigia debe utalii wa kitabibu (medical tourism) ili miundombinu inayoboreshwa iweze kuhudumia watu wanaokuja kutoka nje ya nchi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro alisema mkutano huo umehudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Akielezea mafanikio ya taasisi ya Benjamin Mkapa, Dkt. Senkoro alisema kupitia utoaji wa huduma za afya, wameweza kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 32 na wametoa ajira zaidi ya 13,000 kwenye sekta ya afya.

No comments: