Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, akizungumza wakati akifungua mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura Na. 410, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura NA. 103 na Matumizi sahihi ya Takwimu ulioandaliwa na Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji Mtumba Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, akizungumza wakati wa mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura Na. 410, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi,Sura NA. 103 na Matumizi sahihi ya Takwimu ulioandaliwa na Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji Mtumba Dodoma, ambapo umehusisha Kanda ya Kati katika Mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa.
Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (katikati), Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo (wa kwanza kushoto), Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Mhe.Fadhili Chibago, kutoka kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Kaspar Mmuya na Kamisha wa Idara ya Sera na Ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha Dkt. Frederick Mwakibinga wakiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi baada ya kumaliza kwa mkutano.
Baadhi ya Warishiki wa mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura Na. 410, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi,Sura NA. 103 na Matumizi sahihi ya Takwimu ulioandaliwa na Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji, Mtumba Dodoma, ambapo umehusisha Kanda ya Kati katika Mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Dodoma)
Na Josephine Majura, WF, Dodoma
Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Wakuu wa Idara ya Mipango wametakiwa kutumia mafunzo waliyoyapata kuhusu Sheria mpya ya ununuzi, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na Matumizi sahihi ya Takwimu wakati wa utekelezaji majukumu yao na kuwa mabalozi kwa wengine ambao hawajapata fursa hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, wakati akifungua mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura Na. 410, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi,Sura NA. 103 na Matumizi sahihi ya Takwimu ulioandaliwa na Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji,Mtumba, Dodoma.
Alisema kuwa Sheria mpya ya Ununuzi imejikita zaidi katika kulinda maslahi ya Taifa hususan katika kuwanufaisha watanzania, ambapo kumewekwa upendeleo kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
“Makundi hayo yametengewa asilima thelathini ya bajeti ya ununuzi ya kila taasisi ya umma lengo kuu likiwa ni kuyawezesha makundi hayo kushiriki katika zabuni za umma na hatimaye yaweze kukuza kipato chao pamoja na kujenga uwezo”, alisema Mhe. Senyamule.
Aliongeza kuwa upande wa miradi ya PPP pamoja na mambo mengine, Sheria ya PPP sura 103 imefanyiwa marekebisho kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika kutekeleza miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta ya Binafsi.
Mhe. Senyamule alifafanua kuwa Sheria hiyo inaruhusu Wawekezaji katika miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyokuwa vya kikodi, sawa na wale wanaopata vivutio chini ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania, Sura 38.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo alisema kuwa Wizara ya Fedha inaendesha mikutano kwa watendaji wa Serikali waliopo katika ngazi za Mikoa pamoja na Halmashauri za Majiji, Miji na Wilaya.
“Serikali imeona changamoto mbalimbali zinazohusu utekelezwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410, Sheria ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi pamoja na matumizi sahihi ya takwimu zinazoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu,”alisema Bi. Omolo.
Alisema kuwa Mkutano huo umehusisha mawasilisho ya mada tatu, ikiwemo utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na matumizi sahihi ya takwimu.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ununuzi Manispaa ya Singida, Bw. Simon Haule, aliipoongeza Serikali kwa kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni zake.
“Kupitia mafunzo haya, tunaahidi kuwa Mabalozi wazuri kwa wenzetu na tutawafundisha Watendaji wengine katika Taasisi tulizotoka ambao hawajashirikia mafunzo haya ili lengo la Serikali liweze kufanikiwa kupitia sisi”, alisema Bw. Haule.
Mkutano huo umewashirikisha Wakuu wa Taasisi mbalimbali wa Wizara za Kisekta, Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Wakuu wa Idara ya Mipango iliyojumuisha Kanda ya Kati katika Mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa.
No comments:
Post a Comment