ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 23, 2024

WAANDISHI WASAIDIZI NA WAENDESHAJI WA VIFAA VYA BAYOMETRIKI 92 WAAPISHWA SIMANJIRO


Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Waandishi Wasaidizi na Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki 92 kutoka kata nne kati ya 18 za Jimbo la Simanjiro wameapishwa kabla ya kuanza kwa mafunzo ya siku mbili kwa watendaji hao wa uandikishaji yanayofanyika katika mji mdogo wa Mirerani. 
Kwa mujibu wa Afisa Mwandikishaji Msaidizi wa Jimbo la Simanjiro, Dkt. Swaleeh Athuman Masaza, Washiriki wa mafunzo hayo wanatoka kata za Mirerani, Shambarai, Naisinyai, na Endamtu.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imetenga vituo vinne kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa Waandishi Wasaidizi na Waendeshaji wa Vifaa vya bayometriki. Vituo vingine ni pamoja na kituo cha Ferrat, ambacho kinatoa mafunzo kwa washiriki kutoka kata tano, Nyumba ya Mungu yenye kata tatu, na Orkesumet inayojumuisha kata sita.
Mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kufanyika kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Wilayani humo kuanzia tarehe 25 Septemba 2024 hadi tarehe 1 Oktoba 2024.

Pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Simanjiro, uboreshaji wa Daftari pia utafanyika katika kata za Kiteto, na Halmashauri ya Mji wa Mbulu kutoka mkoa wa Manyara.  Pia uboreshaji wa Daftari utafanyika katika mkoa wa Singida, pamoja na Halmashauri za Jiji la Dodoma, Chamwino, Kongwa, na Bahi, zote kutoka mkoa wa Dodoma.
Dkt. Masaza amewataka Waandishi Wasaidizi na Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi pindi uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika eneo hilo utakapoanza.
"Nawasihi mzingatie mafunzo mtakayoyapata ili mwende mkatekeleze majukumu yenu kwa weledi na ufanisi mkubwa," amesema Dkt. Masanza.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kumalizika kesho, ambapo washiriki watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa jukumu la uboreshaji wa Daftari ikiwa ni pamoja na namna ya kutumia vifaa vya bayometriki watakapokuwa katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.

No comments: