Saturday, October 12, 2024

JUKWAA LA WANAWAKE KATIKA USAFIRI WA ANGA LATEMBELEA KITUO CHA WATOTO YATIMA CHA ROLINA


Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa Kike Duniani, Jukwaa la Wanawake katika Usafiri wa Anga Tanzania (WIA-TZ) kwa kushirikiana na Jukwaa la Viongozi katika usafiri wa Anga Afrika (Afican Leaders in Aviation-ALA) wametembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Rolina kilichopo Kwa Sadala mkoani Kilimanjaro na kutoa elimu na uelewa wa sekta ya Usafiri wa Anga.
Akizungumza katika ziara hiyo, Khodana Davhana Mwanzilishi mwenza wa Jukwaa la Viongozi katika Usafiri wa Anga barani Afrika, ameeleza kuwa wanatembelea nchi mbalimbali barani Afrika hususani katika shule na vituo kwa lengo la kuhamasisha vijana hasa wa kike kujiunga na sekta ya usafiri wa anga.
Amesisitiza kuwa masomo yoyote ikiwemo sheria, biashara, udaktari, sayansi n.k yatamuwezesha kijana wa kike kujiunga na sekta ya anga.

Wanachama wa WAI – TZ Bi Upendo Mwaibale Afisa mtoa taarifa za anga na Bi Fatma Kawale, Afisa Uongozaji Ndege walitoa elimu ya usafiri wa Anga na kuwahimiza vijana hasa watoto wa kike kuchukua masomo ya Sayansi, Teknolojia, Hesabu na Uhandisi ili waweze kuingia katika sekta ya Usafiri wa anga, lakini pia waliwahimiza kuishi ndoto zao ili kufikia malengo yao.

Zawadi mbalimbali zimetolewa na Jukwaa kwa vijana ikiwemo vitabu ili kuwajengea uelewa mpana zaidi kuhusiana na sekta ya usafiri wa anga na fursa zilizopo katika sekta.


















No comments: