Sunday, October 13, 2024

MAZRUI AHIMIZA KUSOMEA KADA YA GANZI NA USINGIZI


Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amewashauri vijana wanaosomea kada ya afya kutumia fursa ya kusomea kada ya ganzi na usingizi ili kukidhi hitaji la nchi kwa wataalam wa kada hiyo ambao kwa sasa wapo wachache.

Ushauri huo aliutoa na alipozungumza na waandishi wa habari kuelekea siku ya wataalamu wa ganzi na usingizi duniani ambapo amesema Zanzibar bado inakabiliwa na uhaba wa wataalamu hao.
Amesema Kada ya Ganzi na Usingizi bado inahitaji wataalamu kutokana na umuhimu wake katika sekta ya afya nchini na serikali ya mapinduzi Zanzibar imejidhatiti kuwasomesha wataalamu hao na kuwawekea mazingira mazuri pamoja na maslahi yao.
Hata hivyo Waziri Mazrui amesema kuwa milango ya wizara ipo wazi kuwapa ushauri vijana wanaotaka kujiendeleza katika taaluma ili waweze kuchagua kada hiyo ya ganzi na usingizi.
Amefahamisha kuwa Zanzibar ina wataalamu bingwa wa ganzi na usingizi wanne wataalamu wa ngazi ya shahada ya kwanza 2 na ngazi nyengine 18 Unguja na Pemba ambao wanatengeneza idadi ya wataalamu 49.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ganzi na Usingizi katika Hospitali ya Mnazimmoja Dkt Mwadini Maalim Simai amesema wanafanya jitihda mbali mbali kuona fani hiyo inakuwa na wataalamu wengi zaidi ili kufanikisha utoaji wa huduma katika Hospitali.
Siku ya ganzi na usingizi huazimishwa kila ifikapo tarehe 16 ya mwezi wa 10 ya kila mwaka ambapo Zanzibar itaadhimisha siku hii kwa mara ya kwanza.

No comments: