Friday, October 11, 2024

KAMATI ZA PEMBEJEO ZA WILAYA ZATAKIWA KUHAMASISHA USAJILI WA WAKULIMA ILI KUNUFAIKA NA MBOLEA ZA RUZUKU


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akizungumza na hadhira iliyoshiriki ufunguzi wa maonesho kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayofanyika kwa siku 4 katika viwanja vya Stendi ya zamani vilivyopo Babati mkoani Manyara tarehe 10 Oktoba, 2024

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent akizungumza na hadhira iliyoshiriki ufunguzi wa maonesho kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayofanyika kwa siku 4 katika viwanja vya Stendi ya zamani vilivyopo Babati mkoani Manyara tarehe 10 Oktoba, 2024

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo akizungumza na hadhira iliyoshiriki ufunguzi wa maonesho kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayofanyika kwa siku 4 katika viwanja vya Stendi ya zamani vilivyopo Babati mkoani Manyara tarehe 10 Oktoba, 2024

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga (kushoto) akisalimiana na viongozi walioshiriki ufunguzi wa maonesho kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani, katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Joel Laurent tarehe 10 Oktoba, 2024 Babati Mkoani Manyara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent akizungumza na wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Uvuvi na Kilimo walipotembelea banda la Mamlaka siku ya ufunguzi wa Maonesho kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Dunia tarehe 10 Oktoba, 2024 mkoani Manyara

Na Mwandishi wetu Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amezitaka kamati za pembejeo za wilaya kwa kushirikiana na wenyeviti wa wilaya kuhakikisha wakulima wanajisajili kwenye daftari la mkulima na wale waliojiandikisha msimu uliopita wanahuisha taarifa zao ili wasipitwe na fursa ya mbolea za ruzuku.

Sendiga ametoa wito huo tarehe 10 Oktoba, 2024 alipokuwa akifungua maonesho ya siku nne yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA) kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Oktoba, duniani kote.

Sendiga amesema, awali wakulima walikuwa wakihofia kuwa watakapojiandikisha watatozwa kodi, watanyang’anywa mashamba yao lakini baada ya elimu kutolewa na na viongozi wa mikoa wakiongozwa na wakuu wa mikoa sasa wananchi wameelewa wanajitokeza kujisajili.

Amesema, ili kuhakikisha mbolea zinafika vijijini wafanyabiashara wanawajibu kuhakikisha wanafikisha bidhaa hizo vijijini ili kufikisha huduma hiyo karibu na wakulima.

“Uwekaji wa mbolea mijini, makao makuu ya wilaya, makao makuu ya mikoa, hapo hakuna wakulima wakulima wako vijijini, kwa hiyo wafungue maduka ya pembejeo za kilimo vijijini ili kuwapunguzia wananchi mzigo mzito wa kuja kuchukua mbolea mjini na baadaye wanapata shida ya kusafirisha kwa mabasi inayopelekea gaharama kuongezeka na kuondoa umuhimu wa ruzuku iliyowekwa na serikali” Sendiga amesisitiza.

Ameiomba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuhakikisha bei elekezi zinazotolewa zinaakisi uhalisia wa jiografia na miundo mbinu ya mikoa kutokana na mikoa kuwa mbalimbali ambapo jiografia yake ni ngumu na hivyo kupelekea baadhi ya wananchi kushindwa kunufaika na ruzuku iliyowekwa kwenye pembejeo hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo amesema licha ya Mamlaka kudhibiti biashara ya mbolea nchini Mamlaka imekuwa ikijikita katika kutoa elimu ya mbolea kwa wakulima.

Amesema kwa kipindi kirefu kumekuwa na mkazo wa kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini lakini Mamlaka iinahakikisha elimu ya mbolea inaelekea maeneo mengine ya nchi ili kuwezesha wakulima kuongeza uzalishaji.

Amewasihi wananchi wa Babati na maeneo jirani kutumia maonesho hayo kujifunza kutoka kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa mbolea waliopo katika viwanja hivyo vya maonesho.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amesema, kupitia maonesho haya wakulima na wananchi watapata fursa ya kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na maeneo mengine yatakayowasaidia kuongeza uzalishaji.

Amesema, mbolea ni moja kati ya pembejeo muhimu zinazohitajika katika uzalishaji wa mazao, wakati mbegu bora zikichangia takribani asilimia hamsini ya uzalishaji wa mazao mbolea huchangia kati ya asilimia ishirini hadi arobaini na asilimia zinazobaki hutokana na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo kwa jumla.

Amesema, Mamlaka inaamini kupitia maonesho hayo wakulima na wadau wengine watapata wasaa wa kujifunza na kubadilishana tekinolojia katika kuimarisha matumizi sahihi ya mbolea nchini.

Amesema, maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanaambatana na matukio mbalimbali ikiwemo kongamano la kwanza la mbolea litakalofanyika kwa siku mboili yaani tarehe 11 na 12 Mkoani Dodoma.

Kwa upande wa Manyara Maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya wadau katika mnyororo wa thamani lakini pia siku ya kilele itakayoadhimishwa tarehe 13 Oktoba, 2024 itaambatana na matukio ya mbio za ridhaa (fun run), upandaji wa miti na halfa ya kufunga maadhimisho hayo itakayofanywa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb)

No comments: