ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 8, 2024

WAZIRI MAZRUIA ASISITIZA NIDHAMU NA UWAJIBIKAJI WIZARA YA AFYA





Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amewataka watendaji wa wizara hiyo kuongeza nidhamu ya utendaji kwa lengo la kukuza uwajibikaji ufanisi pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja ili kufikia malengo ya Serikali kupitia Wizara hiyo.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya udhibiti wa viashiria hatarishi, uhujumu uchumi, sheria za utumishi wa umma pamoja na huduma kwa wateja huko Madinatul Bahri Mbweni Zanzibar amesema kufanya hivyo kutaongeza kasi ya kupunguza mapungufu yaliyomo kwenye utendaji wa wizara hiyo.
Amesema kwa muda sasa wizara ya Afya licha ya kupewa imani kubwa na serikali katika utoaji wa huduma lakini bado ufanisi ni mdogo jambo linalosababishwa na watendaji kutoelewa sheria na kanuni za Wizara hiyo hivyo kutolewa kwa mafunzo hayo yatasaidia kwa watendaji kufanya kazi kwa mujibu wa sheria kanuni na miongozo ili kwa lengo la kukuza ufanisi kwenye maeneo yao.
Sambamba na hayo amekemea tabia ya baadhi ya wakuu wa taasisi, vitengo na idara za wizara hiyo kutowapangia kazi baadhi ya watendaji wao jambo linalodumaza taaluma za watendaji hao na kukosa nafasi ya kuchangia katika maeneo yao ya kazi.
Akigusia suala la migogoro Waziri Mazrui amesema migogoro mingi inatokana na watendaji kutoelewa vyema sheria na kanuni za utendaji wa kazi, hivyo kutolewa kwa mafunzo hayo yataendelea kutia uelewa na kupunguza mambo hayo.
Aidha amewapongeza waandaji wa mafunzo hayo kwa kuweka mada ya huduma kwa wateja japo bado wizara haijafikia utendaji unaotakiwa katika jambo hilo hivyo mafunzo hayo yatakwenda kutoa uelewa mpana kwa watendaji katika kulifikia na kulitekeleza linavyotakiwa kwa jamii.
“Mimi napenda kufanya kazi na watu wanaofanya kazi kwa umoja na mshikamano kinyume na hivyo tutaharibikiwa”, alisema Waziri Mazrui.
Katibu mkuu Wizara ya Afya Dk Mngereza Mzee Miraji amesema lengo la kuandaliwa kwa mafunzo hayo ni kuhakikisha watendaji wa wizara hiyo wanafanya kazi kwa kanuni pamojanna kufuata sheria zitakazoongeza ufanisi katika kufikia malengo ya serikali kupitia wizara hiyo.
Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Wizara ya Afya Zanzibar na kushirikisha wakuu wa taasisi, idara pamoja na vitengo vilivyomo kwenye wizara hiyo.

No comments: