Saturday, December 21, 2024

NSSF YAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KUTUNZA MAZINGIRA KWA KUPANDA MITI JIJINI DODOMA


 *Yapanda miti eneo la Njedengwa, 

*Mkuu wa Mkoa ipongeza  NSSF kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza mazingira 

Na MWANDISHI WETU,
DODOMA. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeunga mkono kwa vitendo juhudi za Serikali za kulifanya jiji la Dodoma kuwa kijani kwa kupanda miti katika eneo la mradi la uwekezaji wa jengo la ofisi na jengo la kitega uchumi la NSSF lililopo kiwanja namba 3 kitalu F, Njedengwa, Dodoma.

Akizungumza mwishoni mwa wiki mara baada ya wafanyakazi wa NSSF wakiongozwa na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema Mfuko unatambua umuhimu wa kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama anavyosisitiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“NSSF tumeona tupate nafasi ya kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali yetu ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yupo mstari wa mbele kuhamasisha utunzaji wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kupanda miti,” amesema Bw. Mshomba.

Amesema lengo la NSSF ni kupanda miti katika maeneo mbalimbali hususan kwenye Ofisi zilizopo mikoa yote Tanzania Bara.   

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary ameishukuru NSSF kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupanda miti na kuwa suala la upandaji miti ni mpango ulioasisiwa na viongozi wa kitaifa akiwemoa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa mazingira na upandaji wa miti.

“Jambo hili mlilolifanya NSSF ni kuunga mkono kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameianzisha na anatamani kuona Dodoma ikiwa ya kijani kabisa,” amesema Mhe. Rosemary.

Ameipongeza NSSF kwa kupanda miti na kuunga mkono juhudi hizo za Serikali katika utunzaji wa mazingira ambapo kwa nyakati tofauti tofauti Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa akitilia mkazo utunzaji wa mazingira na mwaka 2022, alizindua rasmi mpango wa Dodoma ya kijani.

Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema juhudi za kupanda miti katika Mkoa huo zimeongezeka na katika mpango mkakati wa mazingira, Dodoma imewekewa mkazo katika upandaji miti ambapo kila kaya inatakiwa kuwa na miti mitano na taasisi za umma ziwe na miti 100.

“Mlichokifanya NSSF kupanda miti kabla hamjaanza ujenzi ni jambo jema sana kwani suala la utunzaji mazingira ni mpango wa Serikali na championi wa jambo hili ni Rais wetu,” amesema Mhe. Rosemary.



No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake