ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 23, 2024

RAIS WA ZANZIBAR DK.HUSSEIN MWINYI AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA UWANJA MAISARA SULEIMAN UNGUJA.IKIWA NI SHAMRASHAMRA ZA MIAKA 61 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inakusudia kujenga kiwanja chengine kikubwa cha kisasa chenye hadhi ya kimataifa, kitakachotumika kwenye michuano ya AFCON, mwaka 2027.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa viwanja vipya vya michezo Maisara (Maisara Sports Complex), Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza Serikali imelenga kujenga viwanja vya kisasa vya michezo kila wilaya pamoja na “Sprots Academy” kila Mkoa.

“Tuna dhamira ya kweli ya kujenga uwanja wa kisasa wa AFCON utakao fanana na ule wa “Old Traford” wa Manchester United ya Uingereza” Alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, ameeleza Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Kenya na Uganda watakuwa wenyeji wa michuano ya AFCON mwaka 2027.
Dk. Mwinyi amesema Serikali pia inakusudia kufanya marekebisho makubwa ya viwanja vya Gombani Kisiwani Pemba na Uwanja wa Mao Tse Tung, Unguja lengo ni kuwa na viwanja vya kisasda vyenye hadhi vitakavyokuwa chachu ya kuwainua vijana kimichezo.

Ameongeza kuwa dhamira nyengine ya Serikali ni kujenga kiwanja cha mpira wa ufukweni (Beach soccer) kwa hadhi ya kimataifa na kujenga bwawa kubwa la kuogelea (Swimming pool) lenye hadhi ya Olympic, (Olympic size Swimming pool)

Amebainisha kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisononeshwa kwa kuwepo viwanja vibovu vyenye vumbi na matope ambavyo vijana walivitumia kuchezea michezo mbalimbali ikiwemo soka, alieleza hali hiyo imepitwa na wakati, hivyo serikali imejiandaa kujenga viwanja vipya ili kutoa fursa kwa vijana kinua vipaji vyao na ushindana kimataifa.

Ameeleza bado Zanzibar ina nia ya kurudi tena kuwa mwanachama wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) hivyo ujenzi wa viwanja hivyo ni chachu ya itakayoleta ushawishi wa kupata uanachama huo.

Amefahamisha kuwa kuna kila sababu ya Zanzibar kuwa mwanachama wa CAF kwa sababu ina timu mahiti ya “Zanzibar Herros” inayoweza kuleta ushindani na kuleta vikombe nchini.

Amesema, lengo ni kuongeza vipaji ili Zanzibar iwe mshindani wa kimataifa katika nyanja mbalimbali za michezo.

Akizungumzia uwanja wa mpya wa Maisara (Maisra Sports Complex) aliouwekea jiwe la msingi, Rais Dk. Mwinyi ameishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa kusimamia ipasavyo, maendeleo ya ujenzi huo ambao kwa kiasi kikubwa utaimarisha sekta ya michezo nchini.

Pia Dk. Mwinyi ameeleza kuwepo kwa viwanja vya mpira wa kikapu (basketi ball), mpira wa wavu (volleyball), mpira wa mikono (hand ball) na mchezo wa “Long tennis” kutatoa mazingira bora kwa vijana kujifundisha michezo hiyo na kuzalisha vipaji zaidi.

Aidha, amefurahishwa kuwepo kwa kituo cha mazoezi ya viungo kiwanjani hapo (fitness center) pamoja na viwanja vya kufurahishia watoto (Children playground).

Akiizungumzia kaulimbiu ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar isemayo “Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo yetu” aliwasihi wananchi kutokubali kufitinishwa ili maendeleo zaidi yaendelee kupatikana katika sekta mbalimbali.

“Bila ya Amani, Umoja na Mshikamano hakuna suala lolote la maendeleo litakalofaikiwa” alibainisha Rais Dk. Mwinyi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amesema wizara itaendelea kutekeleza na kufuata maelekezo na miongozo inayotolewa na Rais Dr. Mwinyi kwa kukamilisha miradi yote inayosimamiwa na Wizara hiyo kwa wakati na mafanikio.

Ameeleza kuwa kinachofanyika hivi sasa katika viwanja vya michezo Unguja na Pemba ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, 2020 -2025 kwa vitendo.

Waziri Tabia pia amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kutunzwa na kulindwa kwa viwanja vyote vinavyoojengwa ili viendelee kutumia kwa miaka mingi iyajo.

Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma Hamad Mbarouk, amesema ujenzi wa viwanja vipya vya “Maisara Spots Complex” ulianza Septemba 2024 na unatarajiwa kukamilika kwake Machi 2025 ambapo kwasasa umefikia asilimi 60 ya ujenzi wake na mkandarasi anaendeleza ujenzi huo kwa kasi inayoridhisha.

Amesema, Ujenzi wa viwanja vipya vya michezo vya Maisara ni miongoni mwa ujenzi wa viwanja 17 vya michezo Unguja na Pemba vyenye viwango vinavyokubalika na CAF na FIFA.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments: