ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 20, 2024

TCAA YAENDELEA KUIMARISHA MIFUMO YA MAWASILIANO SEKTA YA USAFIRI WA ANGA

  


Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),Kituo cha Arusha Bw. Jackson Ndalu akiwaelezea Wajumbe wa Bodi ya TCAA jinsi shughuli za Uongozaji wa Ndege zinavyofanyika katika mnara wa kuongozea ndege wa Arusha. Ziara hii ya Bodi na Menejimenti inalenga kukagua maendeleo na utekelezaji wa miradi mipya ya TCAA katika Uwanja wa Ndege wa Arusha ikiwemo Radio za Mawasiliano.
Afisa wa Mtoa taarifa za Usafiri wa Anga wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Piniel Laizer, akiwapa maelezo Wajumbe wa Bodi ya TCAA  jinsi mchakato mzima wa huduma hii ya utoaji wa taarifa za usafiri wa anga zinavyotekelezwa katika ofisi ya maelezo ya safari. Ziara hii ya Bodi na Menejimenti inalenga kukagua maendeleo na utekelezaji wa miradi mipya ya TCAA katika Uwanja wa Ndege wa Arusha.

Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wamefanya ziara katika kituo cha TCAA kilichopo Uwanja wa Ndege wa Arusha  kukagua shughuli za uongozaji ndege pamoja na utekelezaji wa miradi.

Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni mradi wa mawasiliano ya sauti wa VHF, ambao umeboresha mawasiliano kati ya marubani na waongozaji wa ndege.

Ziara hiyo iliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Bi. Mtumwa Ameir, ambaye aliipongeza juhudi zilizofanywa na TCAA katika kuboresha sekta ya usafiri wa anga. Alisema, "Tunajivunia maendeleo haya; ni hatua kubwa katika kuhakikisha usalama na ufanisi wa usafiri wa anga nchini."

Kwa upande wake Profesa Siasa Mzenzi, mjumbe wa bodi, alisifu serikali kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga. Alibainisha, "Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, na matokeo yake yanaonekana wazi."

Awali akitoa maelezo, Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi wa Mitambo ya Kuongozea ndege wa TCAA, Zawadi Maalim, alieleza kuwa mamlaka imejizatiti kutunza uwekezaji huu wa miradi na kuhakikisha miradi inayoendelea inakamilika kwa wakati. Alisema, "Tumejipanga kuhakikisha vifaa hivi  vinatumika ipasavyo, vinatunzwa vizuri na miradi yote inakamilika kwa wakati ili kuboresha zaidi huduma zetu."

TCAA imeendelea kuboresha sekta ya usafiri wa anga nchini kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ufungaji wa mfumo wa rada za kuangazia anga na sasa shughuli za uongozaji ndege zinafanyika kwa ufanisi zaidi.


No comments: