ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 13, 2024

WAZEE WAMETAKIWA KUWA MAKINI KATIKA MALEZI YA WATOTO WAO NA KUSIMAMA IMARA KATIKA KUPIGA VITA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA



Waumini wa Dini ya kiislam na wazanzibari kwa ujumla wametakiwa kuwa makini katika malezi ya watoto wao na kusimama imara katika kupiga vita udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto jambo ambalo linaiondolea sifa njema nchi yetu .

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid RABIA AYYUTUL ulipo SHAKANI Wilaya ya Magharibi “ B “ mara baada ya kumaliza Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema ni lazima waumini wa dini zote kushirikiana katika kupambana na Vitendo vya Udhalilishaji dhidi ya watoto hasa katika kipindi ambacho skuli na Madrasa zimefungwa pamoja na kuacha muhali kwa kwenda kutoa ushahidi mahakamani na sehemu za kisheria ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa Zanzibar ni nchi ambayo imetoa wanazuoni wengi ambao waliipigania dini ya Allah kwa kuhimizana mema na kukatazana maovu hivyo inapaswa kila mmoja kwa nafasi yake kushikamana katika kuhakikisha hadhi na heshima ya Zanzibar inarejea hasa katika suala zima la maadili.

Alhajj Hemed amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelelea kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji hasa kwa wanawake na watoto.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewasisitiza wazanzibari na watanzania kwa ujumla kusimama imara katika kuilinda tunu ya Amani na utulivu iliyopo nchini jambo ambalo mataifa mengi duniani wameikosa tunu hio kwa muda mrefu na kuamua kuja Tanzania kufata amani.

Mapema akitoa Khutba katika Swala ya Ijumaa, Sheikh KHALIFA SALIM OMAR amewataka waumini wa Dini ya Kiislam kuishi kwa amani na utulivu na kuachana na vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwani kufanya hivyo kutapelekea kufanya ibada kwa utulivu na kufikia malengo ya ibada hizo.

Amesema kuwa suala la kuitunza amani ni jambo la watu wote kama ilivyo amrishwa katika kitabu kitukufu cha Qur- an na kuhimizwa na mitume yote iliyoshushwa duniani awamu kwa awamu.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe..13.12.2024.

No comments: