Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi
Mzee Joseph Shija mwenye umri wa miaka 75, mkazi wa mtaa wa Azimio katika kata ya Lubaga, Manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia kwa kujinyonga ndani ya nyumba yake. Tukio hilo limetokea Januari 6, 2025.
Diwani wa kata ya Chibe, Mhe. Kisandu John, ambaye pia ni baba mdogo wa marehemu, amesema alipewa taarifa na majirani kuhusu tukio hilo.
“Majirani waliona nzi wengi kwenye dirisha la nyumba yake, jambo ambalo lilishangaza na kuwalazimu kuwasiliana na familia,” amesema Mhe. Kisandu.
Baada ya taarifa hizo, Mhe. Kisandu alifika eneo la tukio na kutoa taarifa kwa polisi.
Polisi walivunja mlango wa nyumba hiyo na kugundua mwili wa mzee Shija ukiwa umejinyonga kwa kutumia kamba aliyofunga kwenye paa la nyumba yake.
Marehemu alikuwa akiishi peke yake baada ya mkewe kuugua kwa takribani miaka minne.
Familia ya marehemu imesema kuwa kifo hiki si cha kwanza katika familia yao, kwani Mzee Shija anakuwa mtu wa nne kufariki kwa kujinyonga.
Historia hiyo inajumuisha mama yao, kijana mmoja kutoka Kahama, na binti mwingine wa familia hiyo ambao walijinyonga kwa sababu ambazo bado hazijajulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua marehemu kwa muda mrefu.
Kamanda Magomi amekemea vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kusisitiza kuwa kujinyonga si suluhisho la changamoto za maisha.
“Ni muhimu kwa jamii kuachana na hali hii, kwani haionyeshi mfano mzuri kwa watoto na jamii kwa ujumla,” amesema Kamanda Magomi.
Mazishi ya Mzee Joseph Shija yamefanyika leo katika mtaa wa Azimio, kata ya Lubaga, Manispaa ya Shinyanga.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake