Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe SACP Augustino Ignace Senga akiongea na baadhi ya wananchi wa wilaya ya Momba.
Ikiwa leo ni Januari Mosi mwaka 2025 Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanasherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.Kauli hiyo imetolewa Januari 01,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Ignace Senga mara baada ya mazoezi ya kila siku na amesema kuwa Jeshi hilo limejipanga kuhakikisha sherehe ya mwaka mpya inapita salama kwa kuendelea kuimarisha doria za miguu, magari na Mbwa wa Polisi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
Aidha, Kamanda Senga amesema baada ya sikukuu ya Krismasi Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limejipanga vizuri katika sikukuu ya mwaka mpya ikiwa ni pamoja na kuusherekea kwa amani kwa kuimarisha ulinzi katika nyumba za ibada na doria za mtaa kwa mtaa ili jamii iendelee kuwa salama katika kipindi chote cha sikukuu hii.
Vilevile, katika kuhakikisha usalama barabarani una kuwepo, Kamanda Senga ameeleza kuwa kipindi hiki, Jeshi la Polisi Mkoani humo litawachukulia hatua kali wale wote ambao watakiuka sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwafungia leseni na kuwafikisha mahakamani.
"Niwatake wananchi wa Mkoa wa Songwe kuwa na ulinzi jirani pindi mnapoondoka nyumbani msisahau kumuacha muagalizi katika maeneo yenu ili kuweza kuendelea kuwa na usalama mpaka pale mtakaporudi" alisema Kamanda Senga.
Kamanda Senga alisistiza kuwa doria hizi ni endelevu ndani ya Mkoa wa Songwe kwa lengo la kuendelee kutimiza jukumu mama la Jeshi la Polisi la Kulinda raia na mali zao na alitoa wito kwa wananchi kutii sheria bila shuruti na kuacha tabia ya kufanya vurugu za aina yoyote badala yake washerehekee kwa amani na utulivu.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake