Wednesday, January 1, 2025

SITA WAFARIKI BAADA YA GARI YAO KUPINDUKA NA KUWAKA MOTO.



Na John Walter -Ruvuma
Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma limetoa ufafanunuzi kufuatia ajali ya gari aina ya Toyota Prado lenye Namba za usajili T 647 CVR iliyotokea baada ya gari hilo kupinduka na kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu sita ambao walikuwepo ndani ya gari hilo.

Akizungumza na Vyombo vya Habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya amesema kuwa chanzo cha ajili hiyo ni mwendokasi wa dereva wa gari hiyo kuikosa kona na kupelekea kugonga mwamba wa jiwe uliopo pembezoni mwa barabara hiyo ya mbinga-Nyasa, kisha kupinduka na kuwaka moto .

Ni kwamba Disemba 28, 2024 majira ya Saa moja asubuhi katika Kijiji cha Buruma Kata ya Mpapa Wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, katika barabara ya mbinga -Nyasa, gari hiyo ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Vicent Milinga ambaye ndio mmiliki wa gari hilo, ambalo lilikuwa likitokea kijiji cha Lumaru na kuelekea Wilaya ya Nyasa liliacha njia baada a kuikosa kona na kugonga mwamba wa jiwe uliopo pembezoni mwa barabara hiyo na kupinduka kisha kuwaka moto na kusababisha vifo vya abiria sita walikuwepo katika gari hilo ambao walikuwa wakielekea wilayani Nyasa kwa ajili ya kuhudhuria semina ya BVR.

Halikadharika Kamanda Chilya ameorodhesha majina ya abiria waliokuwepo katika ajali hiyo ambao ni, Vicent Milinga-Dereva na Mmiliki wa gari na mkazi wa Lumaru, Damas Nambombe-Mwalimu wa Shule ya Msingi Lumaru wilayani Nyasa, Dominick Albert Ndau -Mwalimu wa Shule ya Msingi Lumaru wilayani Nyasa, Judithi Joseph Nyoni-Mwalimu wa Shule ya Msingi Lumaru wilayani Nyasa, John Silvester Mtuhi -Mwalimu wa Shule ya Msingi Lumala wilayani Nyasa, Boniphace Bosco Makupnda - Mhitimu wa Kidato cha Sita mkazi wa kijiji cha Lumaru.

Miili ya Marehemu wote imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kwa ajili kukamilisha uchunguzi wa kisayansi ili ndugu waweze kutambua ndugu zao.

Pamoja hilo pia Kamanda Chilya amewataka Wananchi kutambua umuhimu wa kuokoa maisha pale panapowezekana badala ya kushuhudia maafa yakitokea na sio kuchukua video huku watu wakiangamia kitendo ambacho sio kizuri kwa jamii na Nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake