Friday, January 3, 2025

WATUHUMIWA 9,985 WA MAKOSA MBALIMBALI YA UHALIFU WALIKAMATWA NA KUFIKISHWA MAHAKAMANI MKOANI MBEYA




JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha 2024 lilifanikiwa kwa kiwango kikubwa kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kuhakikisha linalinda raia na mali zao, linadhibiti ajali za barabarani na kukamata watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo mauaji, kujeruhi, unyang’anyi wa kutumia silaha, uvunjaji, wizi na matukio mengine ya kimaadili kama vile matumizi ya dawa za kulevya, pombe moshi, bidhaa za magendo na usafirishaji haramu wa binadamu.

Kwa kipindi cha 2024 jumla ya watuhumiwa 9,985 wa makosa mbalimbali ya uhalifu walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Jumla ya makosa yote ya jinai yaliyoripotiwa yalikuwa 22,049 ukilinganisha na kipindi kama hicho 2023 yalikuwa 23,754 hivyo kuna pungufu la makosa 1,705 sawa na asilimia 7. [7%].

Kwa upande wa usalama barabarani, jumla ya makosa yote ya ukiukwaji sheria za usalama barabarani yaliyokamatwa yalikuwa 115,216 ukilinganisha na kipindi kama hicho 2023 yalikuwa 115,820 hivyo kuna pungufu la makosa 604 sawa na asilimia 0.5

Maduhuli ya serikali yaliyokusanywa Mkoa wa Mbeya kutokana na makosa ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani yalikuwa Tshs 3,456,480,000/= ukilinganisha na kipindi kama hicho 2023 yalikuwa Tshs 3,351,680,000/= hivyo kuna ongezeko la Tshs 104,800,000/=.

Vile vile, jumla ya madereva 28 walifungiwa leseni za udereva kutokana na makosa hatarishi ya usalama barabarani ikiwemo mwendo kasi, kuyapita magari mengine katika maeneo hatarishi na kusababisha ajali za vifo au majeruhi. Aidha, madereva 29 walifikishwa mahakamani kutokana na kukiuka sheria za usalama barabarani.

Aidha, jumla ya kesi zote zilizofikishwa mahakamani kwa kipindi cha 2024 zilikuwa 9,825 ambapo kesi 2,769 zilipata mafanikio mahakamani kwa washitakiwa kukutwa na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali ikiwemo kunyongwa hadi kufa, kifungo cha maisha jela, miaka 30 jela na wengine vifungo vya nje. Kesi 7,056 bado zipo mahakamani zikiendelea kusikilizwa katika hatua mbalimbali.

Mwaka 2024 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipata mafanikio makubwa katika oparesheni, misako na doria zilizofanyika katika maeneo mbalimbali kwa kuhusisha vyombo vingine vya ulinzi, wadau wa ulinzi na wananchi ambapo watuhumiwa 220 wakiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi uzito wa kilogram 358 na miche 234 walikamatwa, watuhumiwa 239 wakiwa na pombe haramu ya moshi [Gongo] yenye ujazo wa lita 1,253 na mitambo 9 ya kutengenezea pombe hiyo walikamatwa.

Mafanikio mengine ni pamoja na madini aina ya dhahabu yenye uzito wa kilogram 9 na gram 622.76 yenye thamani ya Tshs 1,515,621,987.03 yalikamatwa, watuhumiwa 6 walikamatwa wote wanaume, Nyara za Serikali zenye thamani ya Tshs 288,925,000/= zimekamatwa na watuhumiwa 31 walikamatwa [wanaume 29 na wanawake 2], Wahamiaji haramu 60 walikamatwa kati yao Ethiopia 43, Malawi 15, Burundi 1 na Rwanda 1 [Wanaume 42 na wanawae 8].

Silaha 12 kati ya hizo gobole 11 na shot gun 1 pamoja na risasi/goroli 63, na baruti kwenye kopo dogo tatu zimekamatwa [watuhumiwa 13 wote wanaume walikamatwa], Silaha moja aina ya Pump Action iliyofutwa namba ambayo iliporwa lindoni Nzovwe Jijini Mbeya April, 2023 ilipatikana na watuhumiwa 02 walikamatwa, pia Bastola moja nambari PX384762 na risasi zake 15 iliyokuwa imeibwa Wilaya ya Chunya ilipatikana na risasi zake na silaha moja pump action namba MV841088 ikiwa na risasi 2 mali ya SUMA JKT iliyokuwa imetelekezwa ilipatikana.

Pia katika kipindi cha mwaka 2024 yalikuwepo matukio ya kuibiwa watoto ambapo mtoto Juliana Kiwelo, mwenye umri wa miezi 2 na nusu aliyeibiwa Kijiji cha Mwakaganga Wilaya ya Mbarali alipatikana akiwa hai na mtuhumiwa Anna Mwakilima [24] mkazi wa Mbuyuni Wilaya ya Mbarali alikamatwa, Mtoto Petro Venansi Mwavilenga, mwenye umri wa miaka 9, Mwanafunzi Shule ya Msingi Soweto darasa la tatu aliyeibwa Wilaya ya Chunya alipatikana akiwa hai ambapo mtuhumiwa Godfrey Malema [32] mkazi wa Makongolisi alikamatwa na alifikishwa mahakamani na kupatikana na hatia kwenda jela miaka 2, na tukio jingine ni la mtoto Joyce Layson Mkongwi, miaka 5, mwanafunzi wa Shule ya Chekechea ya Isaiah Samaritan aliyetekwa alipatikana akiwa hai ambapo watuhumiwa 3 walikamatwa akiwemo mama mzazi wa mtoto huyo na kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia ya kwenda jela.

Sambamba na hayo, mwaka 2024 yalikuwepo matukio yaliyovuta hisia kwa jamii likiwemo tukio la mauaji lililotokea tarehe 31.03.2024 saa 2:30 usiku huko Kijiji cha Kiwanja, Wilaya ya Chunya. Watu wawili ambao ni Herriet Modest Lupembe [37] aliyekuwa Mwalimu katika Shule ya Msingi Mbugani na Ivon Tatizo [15] aliyekuwa Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Isenyela walikutwa wameuawa kwa kupigwa kitu butu kichwani wakiwa ndani nyumbani kwao.

Katika tukio hilo mtoto Haris Barnaba [6] Mwanafunzi Shule ya Msingi Kengold Chunya [mtoto wa Herriet Modest Lupembe] alijeruhiwa kwa kupigwa kitu butu kichwani hivyo kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu.

Kwa sasa amepona.
Chanzo cha tukio ni mgogoro wa kifamilia ulioambatana na wivu wa kimapenzi baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mzazi mwenzake kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine licha ya kumhudumia ikiwa ni pamoja na kumjengea nyumba. Mtuhumiwa Barnabas Daud Mtewele [33] mfanyabiashara, mkazi wa Mtaa wa Sinza – Chunya alikamatwa na kufikishwa mahakamani. Kesi ipo mahakamani inaendelea.

Pia, tarehe 15.05.2024 saa 11:45 jioni iliripotiwa taarifa ya kupotea kwa mtoto Joyce Layson Mkongwi, miaka 5, Mwanafunzi wa Shule ya Chekechea Isaiah Samaritan ya Jijini Mbeya. Tarehe 24.05.2024 saa 4:00 usiku Polisi wakiwa katika ufuatiliaji wa tukio hilo walimkamata Winfred Martin Komba [36], Mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam aliyekuwa akimtaka baba mzazi wa mtoto huyo aitwaye Layson Mkongwi [35] Mfanyakazi kampuni ya kuuza rangi Gold Stars, mkazi wa Isyesye atoe pesa Tshs 20,000,000/= ili ampate mtoto wake.

Mtuhumiwa alikiri kufanya tukio hilo kwa kushirikiana na Agnes Jacob Mwalubuli [mama mzazi wa mtoto] ambaye ana mahusiano naye ya kimapenzi ikiwa ni njama waliyopanga ili kumshinikiza baba wa mtoto atoe pesa hizo. Mtoto huyo walimchukua tarehe 15.05.2024 huko Isyesye Mbeya na kwenda kumhifadhi kwa Hamida Gaudence Njuu [31] Mkazi wa Simike Mbeya.

Tarehe 24.05.2024 saa 00:45 usiku mtoto huyo alipatikana akiwa salama eneo la Simike Jijini Mbeya nyumbani kwa Hamida Gaudence Njuu kisha baadae kukabidhiwa kwa baba yake mzazi. Watuhumiwa wote watatu walifikishwa Mahakamani. Kesi imemalizika ambapo mtuhumiwa Winfred Martin Komba alipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela miaka 2, Mtuhumiwa Agness Jacob Mwalubili alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha nje mwaka mmoja, Mtuhumiwa Hamida Gaudence Njuu aliachiliwa huru.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kutoa taarifa za wahalifu ili waweze kuchukua hatua ikiwemo kukamatwa. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litawataka baadhi ya wananchi ambao bado wanaendelea na uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi na madhara yake ni makubwa hivyo ni vyema wakatafuta shughuli nyingine za kufanya.


Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake