Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imeanza utekelezaji wa mradi maalumu wa kuimarisha uhifadhi wa aina 57 za miti iliyo katika hatari kubwa ya kutoweka nchini, hatua inayolenga kulinda bioanuwai ya Taifa na kuendeleza matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.
Mradi huo wa miaka mitatu unaojulikana kama Enhanced Conservation of 57 Highly Threatened Tanzanian Tree Species ulizinduliwa jijini Dodoma na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. John Elia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Elia alisema Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa bioanuwai, lakini baadhi ya spishi za miti zinaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa makazi ya viumbe hai na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za misitu.
Alisema Serikali imeamua kuchukua hatua madhubuti za uhifadhi baada ya zaidi ya aina 376 za miti nchini kuorodheshwa katika Orodha Nyekundu ya Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) kuwa katika viwango tofauti vya hatari ya kutoweka.
“Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha spishi hizi zinaendelea kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Elia.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi na Kamishna Msaidizi Muandamizi pamoja na Meneja wa Biolojia ya Mbegu za Miti wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bw. Fandey Mashimba, alisema mradi huo unafadhiliwa na Franklinia Foundation na Missouri Botanical Garden kwa gharama ya dola za Marekani 390,000.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya TFS na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na utahusisha ukusanyaji wa mbegu, uzalishaji wa miche, utafiti wa kisayansi, urejeshaji wa makazi ya asili ya spishi husika pamoja na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa uhifadhi.
Mashimba alisema utekelezaji wa mradi huo utaimarisha juhudi za taifa za kuhifadhi bioanuwai na kuweka msingi wa kuokoa spishi nyingine za miti zinazokabiliwa na changamoto za kutoweka.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wataalamu wa misitu, watafiti na wadau wa uhifadhi kutoka ndani na nje ya nchi.











No comments:
Post a Comment