Na. Mwandishi Wetu,
Dodoma.
MENEJIMENTI ya Wizara ya Maliasili na Utalii ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii Bw. Nkoba Mabula imekutana na kufanya mazungumzo ya kuimarisha uhusiano na uongozi wa Benki ya NMB ukiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali Makao Makuu ya NMB Dodoma Bi. Vicky Bishubo.
Mazungumzo hayo ya Kimkakati baina ya pande hizo mbili yamefanyika leo Julai 27, 2026 katika Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumzia kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Mabula amesema kimekuwa na tija kubwa kwani Benki ya NMB ni wadau muhimu wa Wizara ya Maliasili na Utalii hususani katika kuimarisha maeneo yake makuu ya Utalii na Uhifadhi.
“Ugeni huu wa wenzetu kutoka NMB unadhihirisha namna Wizara ya Maliasili na Utalii inavyozingatia umuhimu wa kukutana na wadau mbalimbali kama sehemu ya kujenga uhusiano wa karibu na pia kuimarisha utendaji kazi wa Wizara kwa wadau na wananchi kwa ujumla,” amesema Bw. Mabula.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali NMB Makao Makuu Dodoma Bi. Bishubo amesema lengo la kutembelea Wizara ya Maliasili na Utalii ni muendelezo wa Mpango wa benki hiyo kutembelea wadau mbalimbali kwa nia ya kuimarisha uhusiano baina ya pande mbili husika.
Amesema kupitia Mpango huo, Benki ya NMB inaendelea kujipambanua kwenye soko na kujenga uhusiano wenye tija baina yake na wadau na hivyo kujiimaarisha zaidi katika mnyororo mzima wa utoaji huduma za kifedha nchini.

No comments:
Post a Comment