Na. Calvin Katera - Arusha.
Zaidi ya washiriki 500 kutoka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ikiwemo Kenya, Uganda, Uingereza na Ujerumani wachagiza utalii wa ndani kwa kushiriki mbio za Arusha Tourism Marathon zilizorindima ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha ikihusisha mbio ndefu na mbio fupi za kilometa 2.5, kilometa 5, kilometa 10 na kilometa 21, leo Julai 12, 2026, jijini Arusha.
Washiriki hao walitumia tukio hilo kama fursa ya kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha, ikiwemo Serengeti ndogo, wanyamapori na ndege mbalimbali, misitu na mandhari ya mlima Meru, jambo lililowapa uzoefu unaounganisha michezo, utalii na uhifadhi.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha Witness Shoo, alisema mbio hizo zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hifadhini, kuhamasisha utalii wa ndani na mchango wa michezo na burudani katika kuzitangaza Hifadhi za Taifa, kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake, Bw. Cornell Magoti, Mkurugenzi na Mwanzilishi ya mbio hizo za Arusha Tourism Marathon alisema lengo la mbio hizo ni kuunganisha sekta ya michezo na utalii kwa kuhamasisha watu kutembelea vivutio vya Tanzania, huku zikichochea uchumi wa eneo kupitia ongezeko la wageni wanaotumia huduma mbalimbali za utalii, malazi na usafiri.
Aidha, washiriki walieleza kufurahishwa na mazingira salama na yenye kuvutia ya hifadhi hiyo, wakisema mbio hizo zimewapa fursa ya kipekee ya kufanya mazoezi huku wakifurahia mandhari ya kipekee ndani ya hifadhi, hali iliyowafanya wengi kuahidi kurejea tena pamoja na familia na marafiki zao kutalii na kujiunga na matukio mengine ya kimichezo na burudani yatakaoendelewa kubuniwa na kuibuliwa.
Arusha Tourism Marathon imejenga msingi na kuwa moja ya matukio muhimu ya utalii wa michezo nchini, ikiiunga mkono jitihada za Serikali kupitia TANAPA na wadau wa sekta ya utalii na uhifadhi, kuongeza idadi ya watalii wa ndani na kimataifa, pamoja na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.











No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake