ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 22, 2026

NAIBU SPIKA SILLO APONGEZA VIONGOZI KWA UBUNIFU WA MANYARA TANZANITE MARATHON

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo


Mbio za Hisani za Manyara Tanzanite Marathon zimefanyika leo mkoani Manyara, zikihudhuriwa na watu mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya nchi pamoja na viongozi mbalimbali, huku lengo kuu likiwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wachanga na watoto njiti.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo, aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio hizo, amepongeza uongozi wa Mkoa wa Manyara kwa ubunifu wa kuanzisha mbio hizo zinazolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya na kuokoa maisha ya watoto wachanga na watoto njiti.

Sillo amesema hatua hiyo ni mfano wa ubunifu unaopaswa kuigwa na maeneo mengine nchini, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii na wadau katika kusaidia kuboresha huduma za afya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Jafari Rajabu, amesema mbio hizo zimeleta tija kubwa katika juhudi za kuokoa maisha ya watoto, akiwataka wananchi na wadau kuendelea kuunga mkono jitihada zinazolenga kuboresha afya ya watoto.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewashukuru wadau wote walioshiriki na kuunga mkono maandalizi ya mbio hizo, akisema ushiriki wao umewezesha kufanikisha azma ya kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto wanaohitaji huduma maalumu za afya.

Baadhi ya washiriki wa mbio hizo wamesema, pamoja na kushiriki kwa ajili ya mazoezi na kuimarisha afya zao, wameona umuhimu wa kuwa sehemu ya harakati za kuchangia maisha ya watoto wachanga na watoto njiti.

Wamesema ushiriki wao katika Manyara Tanzanite Marathon umewapa fursa ya kufanya mazoezi huku wakitoa mchango wa moja kwa moja katika kusaidia kuokoa maisha ya watoto, hivyo kuwataka wananchi wengine kuendelea kushiriki katika matukio yenye malengo ya kijamii na kiafya.



















No comments: