Saeeda Khan anayeshitakiwa kwa kumfanyisha kazi za kitumwa Mwanahamisi Mruke.
DAKTARI mmoja mstaafu wa kike amefikishwa mahakamani nchini Uingereza kujibu mashitaka ya kumshikilia utumwa mwanamke mmoja Mtanzania kwa miaka minne nyumbani kwake akimtumikisha kazi za nyumbani na kumlipa mshahara wa Paundi 10 za Uingereza ambazo ni sawa na sh. 23,000/= za Kitanzania.Saeeda Khan ( 68) anayeishi katika jumba lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja za Kitanzania (Paundi 500,000), anakabiliwa na mashitaka ya kumfanyisha kazi Mwanahamisi Mruke kwa masaa 24 kwa siku akiwa anafanya usafi, kupika na kutunza bustani. Anadaiwa alikuwa akimpa mabaki ya mikate na kumlaza kwenye godoro jembamba jikoni na shuka moja tu bila kujali baridi nchini humo.
Khan na marehemu mumewe ambaye pia alikuwa daktari, walimlipa mwanamke huyo mshahara huo mdogo ambao hata nchini Tanzania wafanyakazi wa ndani wanalipwa mara mbili zaidi yake. Watu hao wanasemekana walimchukua mwanamke huyo na kumpeleka Uingereza mwaka 2006.
Simu zote za Mruke zilikuwa zinafuatiliwa na daktari huyo na alikuwa haruhusiwi kuondoka katika makazi hayo ya kitajiri yaliyoko huko Harrow, Kaskazini-Magharibi mwa jiji la London, bila kufuatana na Khan, mahakama ya Westminster magistrates iliambiwa.
“Aliishi maisha ya umaskini mkubwa kwa miaka kadhaa,” alisema mwendesha mashitaka Malachy Pakenham.
Ilidaiwa kuwa Paundi 40 za ziada kwenye mshahara wake wa kila mwezi zilikuwa ziwe zinapelekwa katika benki moja nchini Tanzania kwa ajili ya kulipia gharama ya elimu ya binti wa Mruke, lakini sehemu kubwa ya fedha hiyo haikupokelewa.
Khan, raia wa Uingereza ambaye ameishi nchini humo kwa miaka 30, anaaminika kuwa mtu wa kwanza kufunguliwa mashitaka ya kuendesha utumwa wa kisasa.
Kesi hiyo iliibuliwa na askari kanzu wa Uingereza baada ya kudokezwa na Wasamaria wema hususani majirani wa daktari huyo.
Hata hivyo, Khan hakusimama kizimbani wakati wa dakika kumi za kusikilizwa kwa kesi hiyo kwani alikuwa anaumwa ugonjwa wa baridi yabisi na hivi karibuni alikuwa amefanyiwa operesheni kwenye magoti yake.
Daktari huyo alikiri kupanga kumwingiza mtu wa nchi za nje nchini kwa ajili ya kumtumikisha kiutumwa nchini Uingereza na kwengineko. Hukumu ya mashitaka hayo ni kifungo cha miaka kumi jela.
Mshitakiwa huyo alipewa dhamana hadi mwezi ujao ambapo kesi itaendelea kusikilizwa. Kabla ya kupelekwa Uingereza, Mruke alikuwa akifanya kazi katika hospitali moja iliyokuwa ikiendeshwa na marehemu mume wa Khan jijini Dar es Salaam.
Biashara ya utumwa ilipigwa marufuku nchini Uingereza tangu karne ya 19. Hata hivyo, nchi hiyo inaendelea kuwa kituo kikubwa cha wanawake wanaouzwa nchi za nje.
Mashirika ya haki za binadamu hudai zaidi ya watu 1,000 hufanyishwa kazi kama watumwa nchini humo.
No comments:
Post a Comment