ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 4, 2010

Facebook, simu za mkononi zinavyoumiza watu katika mapenzi-3

Mungu mpaji wa viumbe vyote, ndiye aliyetoa fursa hii kwangu, ili niitumie kama mwangaza kwako ndugu yangu. Namshukuru sana kwakuwa yeye ndiye kila kitu katika maisha yangu.

Tupo kwenye sehemu ya tatu ya mada yetu. Twende kazi msomaji wangu,kuna kitu kikubwa cha kukusaidia utakachokipata baada ya hapa.

Hebu jiulize, wapenzi wanatengana, wanandoa wanakosa suluhu, kwa sababu ya sms au simu. Ama baadhi wanaishi katika uhusiano wa ‘ilimradi siku zinaenda’, yaani ni mashaka tupu.

Wengine hawana amani, wanawapiga marufuku wenzi wao kushika simu zao au kuzizima muda wote, yote kwa yote ni kukwepa nyeti zao za kucheza mechi za nje, zisigundulike.

Lipo pia, lile kundi ambalo ‘husevu’ majina ‘feki’ katika simu zao ili wasishtukiwe, Husna kuitwa Hussein, Nasra kuandikwa Nassor au Grace kama Gallus. Ama mwanamke kumuandika Joseph kama Josephine, hivyo ni vijimambo tu!

Kama utakumbuka vizuri katika kipengele cha kwanza cha mada hii wiki iliyopita, niliandika ‘KUJIAMINI’. Hapo nilikuwa namaanisha kuwa kama kweli wewe ni muamifu, haina haja ya kujishtukia.

Wapo wenzangu na mimi ambao wakipigiwa simu, badala ya kupokea mbele ya wapenzi wao, wanaweza kufunga safari na kwenda kuongelea maili. Huu nao ni ufisadi!

Daima ukiangalia simu zao, hutakuta sms yoyote, iwe kwenye inbox, outbox, sent item ama katika draft. Ukitazama incoming na outgoing calls, majina hayana mashaka, lakini maongezi yake ni kizaa zaa.

Yeye ni Paulo, amepigiwa simu na Reginald, lakini anaongea kwa mapozi kweli kweli. Chunga unaibiwa, huyo si Reginald, bali ni Regina. Ama Prisca anaongea na Rachel, analegeza sauti, ujue huyo si Rachel ni Richard.

Aidha, katika pointi hii ya kujiamini, ni vizuri pia ukawa mkweli, mpenzi wako akikuuliza mtu aliyekupigia simu, usijikanyage kumjibu. Hata kama ni mwanaume, mwambie ili ajue hakuna kitu kibaya.

Wengine huogopa kuwaambia wenzi wao pale wanapopigiwa simu na wapenzi wa zamani na kuishia kuwadanganya. Unatakiwa kufahamu kwamba hilo ni kosa kubwa, maana akigundua, anaweza kudhani mnaendeleza ‘mambo yenu’ au mnataka kukumbushia.

NAMBA YAKO IWEKEE KUFULI!
Siyo kila mtu barabarani anaweza kukuomba namba na ukampa, hiyo ni tabia mbaya. Mpenzi wako hawezi kufurahia unavyopigiwa simu kila mara na watu wa jinsi tofauti na yako.

Wewe ni mtoto wa kike, umetongozwa umekataa, lakini unaombwa namba unatoa. Ebo! Sasa hapa ulikuwa unakataa au ulitaka tu kumzungusha?
Kwa watoto wa mjini kumpa namba ya simu, inamaanisha umemkubali.

Si mmoja au wawili, wengi siku hizi wananaswa kwa simu tu, yale mambo ya kale ya kwenda kuvizia chini ya mti wa karibu na nyumbani kwao yameshapitwa na wakati.

Mtazamo wangu ni huu, mwanamke anayegawa namba yake ya simu ovyo, huyo ni kicheche, kwa sababu anaruhusu mawasiliano ambayo hayatakiwi. Kakukataa, lakini namba amekupa, kesho ukikaza uzi utampata. Huo ndiyo ukweli!
Umempa namba mwenyewe, akikutumia sms ya mapenzi na mwenzi wako akiiona, utamjibu nini? Acha ufisadi wewe!

USIWE MSIRI
Anayekutaka mwambie mpenzi wako, hapo utayafanya maisha yako yawe na amani siku zote. Hauna dhambi, kila baya linalotaka kukupata, unamfahamisha mpenzi wako.

Ni njia nzuri kwa sababu mtu anayekutaka, unaweza usimpe namba, lakini akaitafuta hata kwa watu wa pembeni, kisha akaanza kukusumbua, lakini unapokuwa umeshamwambia mpenzi wako, hiyo ni ngao.

Siku akiona sms mbaya kutoka kwake katika simu yako, ataipuuzia ama atakuuliza na ukimjibu, atakuelewa na kuondoa mashaka.
HESHIMU HISIA ZA MWENZAKO!
Amekwambia hataki uwasiliane na watu fulani, hebu heshimu anachokwambia, ukifanya vinginevyo au kumzunguka na ‘kusevu’ majina bandia, hapo ni kama unajikaanga kwa mafuta yako mwenyewe.

Kuna siku atajua, halafu amani itatoweka. Anakukataza kuongea na wanaume mara kwa mara, wewe husikii. Hapendi tabia yako ya kupokea simu za wanawake kila saa, unajitia kiburi. Muda si mrefu mtagombana!

Anapowatilia mashaka watu unaowasiliana nao, kisha akakuambia usitishe, kama kweli unampenda, basi acha mara moja! Ukifanya hivyo unakuwa unaheshimu hisia zake.
Wiki ijayo nitachambua athari ya Facebook. Kaa tayari usikose.

No comments: