ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 11, 2010

Facebook, simu za mkononi zinavyoumiza watu katika mapenzi - 4


Hii ni sehemu ya nne na ya mwisho katika mada hii. Tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuwa salama mpaka leo. Yeye ndiye mtenda miujiza, kwa hiyo uwepo wetu duniani, una maana kwamba ametupigania kwa kiwango kikubwa mno.

Nilichagua sehemu hii kuangalia Facebook na namna ambavyo zinaumiza watu kwenye mapenzi. Hii ni baada ya kutumia matoleo mawili mfululizo, kuchambua athari za simu za mkononi peke yake. Nilifanya hivyo nikiwa na mtazamo wa kueleweka kwamba njia hii itasaidia somo kufika sawia.

KUNA UBAYA KATIKA FACEBOOK?
La hasha! Ni matunda ya kukua kwa utandawazi. Mtanzania asiye na pasport, leo anaweza akawa na rafiki Australia ambaye anakuwa anamjua kila kinachoendelea katika Jiji la Sydney. Hakuna gharama kubwa, anajua yote kwa mtindo wa kuchati kwenye ukurasa wa Facebook.

Mtanzania akiwa nje ya nje, akitaka kujua muhtasari wa kile kinachoendela nchini kwake, anaweza kutumia gharama nafuu, kuulizia mazingira na usalama wa taifa kupitia ukurasa wa Facebook. Inapeleka watu katika ulimwengu mpya, inazidisha uhalali wa usemi kwamba dunia ya sasa ni kama kijiji kimoja.

Inasaidia kuongeza wigo wa marafiki. Watu wanaweza kubadilishana mawazo ya kijamii, pia wakapeana uzoefu kwa namna mbalimbali. Inawakutanisha watu kwa njia ya kipekee na kuwafanya wazoeane kabla ya kugeuka marafiki wakubwa. 

INA ATHARI GANI KIMAPENZI?
Facebook imekuwa ikiwafanya baadhi ya wanaume kuona njia ya mkato kupata wapenzi wa mbali. Akaunti yake inajaza marafiki wa kike, hana mpango na wanaume wenzake. Wanakuza wigo wa kunufaika katika ngono.

Msomaji na rafiki yangu, Shadya Ismail aliniandikia ujumbe kwa SMS ambao unasomeka hivi: “Simu ni tatizo lakini huku kwenye Facebook nako ni balaa. Kusema ukweli, mimi nikigundua mpenzi wangu anatumia muda mwingi internet lazima nimfuatilia nijue kinamsumbua nini.”
Nilipomuuliza kwanini, alijibu: “Hakuna amani Facebook.

Mwanaume anaomba urafiki kwa mwanamke na anamkubalia. Wakikutana online wanachati, wanakubaliana baadhi ya vitu na ikiwezekana wanapanga mpaka miadi ya kukutana. Amini kwamba hayo yapo na kuna watu ni mfano.”

Nikamuomba ufafanuzi: “Mapenzi ya siku hizi hayatabiriki, nadhani ndiyo maana tunaambiwa hizi ni nyakati za mwisho. Watu hawajuani lakini wanazoeana kwa kuchati kisha wanakuwa wapenzi. Nasema kwa kujiamini kwa sababu nimetongozwa na wengi.”

Anasimulia alivyotongozwa: “Kuna wanaume watatu waliniomba urafiki kwenye Facebook. Mimi nikikuta ombi nakubali. Siku tukikutana online, tunachati vizuri lakini maswali mengi yanakuwa yale binafsi zaidi, yaani kama vile mtu anataka kukujua sana.

“Nashindwa kutilia hofu, kwahiyo najibu. Mwisho wa yote anamalizia kwa kukutaka kimapenzi. Watu watatu wamenitongoza na kusitisha urafiki nao. Ninao marafiki wawili wa kike, mmoja amewahi kulala kimapenzi na jamaa aliyekutana naye Facebook, alipopata penzi alianza mbele.

“Mwingine mpaka leo anaendelea na mpenzi wake ambaye walikutana Facebook. Lakini huyo mpenzi wake ni mume wa mtu, kwahiyo wanaibana. Hapo utaona ni kwa namna gani fursa za watu kukaribiana kimapenzi zimeongezeka hasa baada ya Facebook kuchanua.”

SHADYA ANASEMA KWELI
Ni ukweli kwamba Facebook inaumiza watu kwenye mapenzi. Idadi ya watu wanaoanzisha uhusiano mpya ni kubwa kila siku kupitia kurasa hizo. Uaminifu umekuwa ukipungua na wasiwasi wa watu kwa wapenzi wao ni kubwa.

Ninao mfano wa jamaa mmoja ambaye kila anapofungua ukurasa wa mwenzi wake, yeye hukimbilia kuangalia marafiki wapya ambao amewasajili. Huumizwa mno anapogundua kuna midume imo kwenye orodha. Wanagombezana lakini ushahidi wa kusaliti haupo.

Mwingine yeye hufuatilia namna mwenzi wake anavyojadiliana na marafiki zake katika mada mbalimbali. Akiona picha ya mpenzi wake imesifiwa mno na mwanaume, anahoji: “Huyu mbona amekusifia sana, ni nani wako? Lazima mtakuwa mnajuana, haiwezekani iwe hivi hivi.”

SULUHISHO
Kila mmoja anatakiwa aishi kwa maumivu ya mwenzi wake. Ni vizuri pia akawa na uelewa mpana kwamba hakuna kitu kibaya kama kumfanya mwenzako kuwa na wasiwasi na wewe. Fanya kila uwezalo lakini hakikisha mpenzi wako anakuamini muda wote.

Atakuamini kama humpi sababu ya kukutuhumu. Haoni tatizo Facebook, rafiki mwenye maneno yasiyofaa, jaribu kumpotezea mapema. Anapofungua ukurasa wako, hakuti kitu kibaya zaidi ya marafiki ambao mazungumzo ni ya kawaida.

Kwanini ulegee kwa kuchati peke yake? Onesha msimamo. Kama wewe ni bachela si vibaya ukianzisha uhusiano lakini ikiwa una mwenzi wako, epuka. Kumbuka kwamba jinsi ilivyo kwako kupata mpenzi, naye hivyo hivyo ni rahisi kunasa wake. Unaona hatari iliyopo?

Uaminifu siyo tu kwamba ni kitu muhimu, bali pia ni nguzo ya uhusiano wowote ule. Ukiwa chanzo wewe ukateleza, utaachwa au ukisalitiwa itakuuma na hata uamuzi utakaouchukua, hautaweza kufidia maumivu uliyoyapata.

No comments: