Jamani tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha tena kupitia safu hii namba moja kwa kuandika makala nzito zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Wiki iliyopita nilizungumzia jinsi unavyoweza kukabiliana na hali ya mpenzi wako kuhisi humpendi au unamsaliti wakati kiukweli hisia zake ni potofu.
Wiki hii nitazungumzia umuhimu wa wapenzi kuhakikisha kila mmoja anachukua nafasi yake kulilinda penzi lao na kulifanya lidumu milele. Nimelazimika kuandika makala haya kutokana na ukweli kwamba, wapo watu waliojaaliwa kupendwa lakini ukiwaangalia hawaoneshi kujali wala kuchukulia kupendwa huko kama bahati kwao.
Nasema ni bahati kwasababu, huko mtaani wapo watu ambao wanaishi maisha yasiyokuwa na furaha kwasababu hawajapata watu wa kuwaita honey, sweetie na majina mengine ya namna hiyo.
Hawana furaha kwakuwa, hawajawapata watu wa kuwabembeleza wanapokuwa katika huzuni, watu wa kuwajali na kuwapa furaha. Ni jambo linalowaumiza wengi sana na ndio maana tunaona kasi ya wanawake kutongoza wanaume inaongezeka tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Sasa hebu jiulize wewe ambaye umebahatika kuwa na mtu anayeonesha kukupenda kwa dhati, unafanya nini kuhakikisha hakuachi? Si suala la kuchukulia juu juu kwa sababu madhara yake katika maisha yako ni makubwa tofauti na vile unavyofikiria.
Waweza kutoonesha kujali leo kwa sababu wapo watu wanaokusumbua wakidai wanakupenda lakini je, una uhakika kwamba wanachokuambia ni kweli? Si kwamba wanakutamani tu? Uliye naye kama kweli unampenda ndiye wa kumng’ang’ania kwa kumjali, kumthamini na kumuonesha upendo wa hali ya juu.
Wengine wasikufanye ukapunguza mapenzi yako kwa mpenzi wako kwasababu ikitokea siku akaamua kukuacha unaweza kujikuta unajuta na kuona bora hata ungeendelea kuwa naye huyo uliyekuwa unamchukulia poa.
Mnatofautiana katika hili na lile? Hiyo ni kawaida katika maisha ya kimapenzi, kikubwa ni kufanya jitihada za kuondoa tofauti zenu haraka kwa kuombana msamaha kila mnapokoseana kisha kuendelea na safari yenu ya mapenzi.
Hata kama mpenzi wako kakukosea, usichukue uamuzi wa haraka, mpe nafasi ya kujiangalia, naamini akigundua kakukosea atakuomba msamaha na wewe usijisikie vibaya kumsamehe.
Akijenga katabia ka’ kukukosea kila mara akitarajia kukuomba msamaha na kusamehewa, mfikirie upya na kuona kama unaweza kuendelea kumvumilia lakini mara nyingi mtu anayekukosea kila wakati penzi lake linakuwa la mashaka.
Hakupi ulichokitarajia? Unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi kuna kitu unachokitarajia kutoka kwa huyo uliyempenda. Wakati mwingine waweza kukosa baadhi ya vitu kutoka kwake lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kumfanyia makusudi ili muachane.
Yeye kama binadamu ana mapungufu, anachokupatia jaribu kuridhika nacho hasa kama anaonesha kukupenda kwa dhati, mengine yatakuja kwa baraka za Mungu.
Yote haya najaribu kuyasema kwasababu kupendwa ni bahati na ukibahatika kuwa kwenye uhusiano unaokufanya angalau ukawa na furaha katika maisha yako, usikubali mambo madogo madogo yakawatenganisha. Uvumilivu uchukue nafasi yake lakini pia kusameheana iwe sehemu ya maisha yenu ya kila siku.
Wazungu wanasema, “Something is better than nothing’ wakimaanisha kwamba, kitu kidogo ulichonacho ni bora kuliko kutokuwa na kitu kabisa. Wewe umebahatika kuingia katika uhusiano kama sio katika ndoa kabisa.
Naamini utakuwa na tofauti kubwa sana na yule ambaye anajitongozesha lakini watu wanampotezea na kama atafanikiwa basi anaweza kujikuta anachezewa kisha anaachwa.
Kumkosa mpenzi kwakweli inauma na inaweza kuyatingisha maisha yako. Lakini sasa kama wewe ni miongoni mwa wale wanaotamani kuwa na wapenzi lakini mpaka sasa hawajabahatika, huna sababu ya kutoa machozi yako. Amini siku itafika na yawezekana utakayempata atakuwa ndiye mwenza wako wa maisha.
Naombeni kwa leo niishie hapo, unachotakiwa kukiingiza katika akili yako leo kupitia makala haya ni kuhakikisha huachani na mpenzi wako uliyempenda kirahisi. Na kama unaona hana nafasi katika moyo wako, msipotezeane muda!
Tuonane tena wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment