Mahakama ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga imemhukumu kwenda jela miaka miwili mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Shule ya Sekondari Konje, Joyce Mganga (15) kwa kosa la kumtetea kijana aliyembaka na kumpa ujauzito.
Mbele ya Mahakama hiyo Septemba 16, mwaka huu, Joyce alijikuta hatiani kwa kile kilichoelezwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Patrick Maligana kuwa alishindwa kuisaidia mahakama dhidi ya kijana Mbaraka Abdallah anayetuhumiwa kwa ubakaji.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka, Brown Lupembe, kesi ya msingi ilikuwa ni tuhuma za msichana huyo kubakwa na kupewa ujauzito, hivyo kufika kwake mbele ya chombo hicho cha sheria ilikuwa ni kutoa ushahidi wa tukio hilo.
Joyce Mganga (15).
Hata hivyo, Joyce anadaiwa kumkera hakimu pale aliposema: “Simfahamu Abdallah (kijana anayetuhumiwa kumbaka) wala sijawahi kumuona.”Kauli hiyo ilitafsiriwa na mahakama kuwa ni njama za makusudi za mwanafunzi huyo kupindisha ukweli kwa lengo la kumtetea mtuhumiwa.
Miguno na taharuki iliibuka ghafla mahakamani hapo pale hakimu alipoamuru msichana huyo mwenye ujauzito wa miezi sita kuwekwa rumande na siku nne baadaye kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya shilingi laki nne.
Hapa ndiyo nyumbani kwao mwananfunzi aliyefungwa jela baada ya kupewa mimba.
Kutokana na hukumu hiyo kufanyika bila wazazi wa mwanafunzi huyo kuwepo mahakamani, Joyce alishindwa kulipa faini hiyo na kupelekwa gerezani kuanza kutumikia kifungo, huku kesi ya msingi ikipangwa kusikilizwa Oktoba 12, mwaka huu.Ukurasa wa hukumu hiyo ulipofungwa, gazeti hili lilianza harakati za kuwatafuta wazazi wa mwanafunzi huyo ambapo Mwandishi Wetu alisafiri mpaka Kijiji cha Kwabaya wilayani Handeni alikokuwa akiishi Joyce na familia yake.
Mbali ya kujionea mazingira magumu aliyokuwa akiishi mwanafunzi huyo na familia yake, mpekua habari wetu alifanikiwa kuzungumza na baba wa msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mhina.
Baba mzazi wa mwanafunzi, Joseph Mhina.
“Hii ni hukumu ya hakimu, kaiona inafaa, ila nina masikitiko makubwa juu ya mwanangu kwa vile hali yake (ujauzito) inahitaji uangalizi wa karibu, naamini mahakama imetoa adhabu kulingana na sheria yao,” alisema Mhina.Kuhusu tukio la binti yake kubakwa na kupewa ujazuto, mzazi huyo alisema limetokana na mazingira magumu ya ulimwengu wa sasa kwenye malezi ya watoto na kuongeza kuwa yeye kama mzazi alikwenda mahakamani kulingana na sheria inavyoelekeza.
Mhina alipotakiwa kuweka wazi kwa nini binti yake alipindisha ukweli mahakamani alisema: “Kwanza ni utoto, lakini kubwa zaidi ni vitisho ambavyo alidai upande wa mtuhumiwa ulikuwa ukivitoa dhidi yao.
“Mimi siishi na Joyce, nafundisha Shule ya Msingi Antakae, nimekuwa nasikia kuna watu wanamtisha mwanangu kwa kusema mtuhumiwa akifungwa watamkomesha pamoja na familia yake, naamini hilo ndilo lililomuogopesha,” alisema Mhina.
Kuhusu kushindwa kumlipia mwanaye faini ya shilingi 400,000 ili asifungwe mzee huyo alisema, limetokana na ukata na kuomba msaada kwa wasamaria wema akiwemo Rais Jakaya Kikwete na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake ‘TAMWA’ wamsaidie.
Kaimu Mkuu wa Shule, Emmanuel Temba.
Naye Emmanuel Temba, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Konje aliyokuwa akisoma Joyce, alionesha masikitiko makubwa kwa kusema hukumu hiyo haikuangalia usalama wa mwanafunzi huyo na hivyo kuomba hatua za haraka zichukuliwe na wanaharakati ili kumtoa kifungoni.“Siyo mtaalamu sana wa masuala ya sheria, lakini ninapotazama umri na hali aliyonayo mwanafunzi wangu nadhani hukumu haikuangalia usalama wake, nafahamu nchi yetu ina wanasheria wazuri, ombi langu ni kwamba wajitokeze kumsaidia,” alisema Temba.
Wakati mwalimu huyo akitoa wito huo kwa jamii nzima, wakazi wa vijiji vitatu vya Kwabaya, Antakae na Konje alikotembelea mwandishi wetu nao wameonesha masikitiko na kuomba msaada wa kisheria.
Wito kutoka dawati la gazeti hili kwa taasisi zote, mashirika na watetezi wote wa haki za binadamu kuungana kwa lengo la kumsaidia msichana huyo ambaye anatumikia kifungo huku akiwa mjazito mwenye umri mdogo.
Habari kwa hisani ya GPL
1 comment:
Wait a minute, god damn it!!! Wtf. Yaani she got raped and then they throw her in jail while pregnant? What's the wisdom in that?
Post a Comment