ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 24, 2010

Kamishna wa TRA amkaanga Mramba

Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba
Tausi Ally
KAIMU Kamishna wa Kodi za Ndani katika Mamlaka ya Mapato nchini(TRA), Christine Shekidele ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa zaidi ya Sh11 bilioni ingeweza kukusanywa kama kodi kama kampuni ya M/S Alex Stewart  Government  Bussines Cooparation isingesamehewa kodi.

Shekidele alitoa madai hayo wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kusibabishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha inayowakabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Shekidele ambaye ni shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka, aliyaeleza hayo jana mbele ya jopo la mahakimu watatu lililokuwa likiongozwa na Jaji John Utamwa, wakati alipokuwa akitoa ushahidi wake dhidi ya kesi hiyo. 

Akitoa ushahidi wake Shekidele alidai kuwa kiasi hicho ambacho kilitakiwa kulipwa na Kampuni ya M/S Alex Stewart kama kodi iwapo isingesamehewa kodi ilitokana na mahesabu yaliyotolewa katika maelezo ya kifedha (financial statement) ya TRA.

Alidai kuwa TRA alifanya uchunguzi baada ya kupelekewa barua na Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), ambayo iliwataka kufanya hivyo, lakini alikuwa hajui kama wanaichunguza kampuni hiyo.

Hata hivyo, Jaji Utamwa aliiahirisha kesi hiyo hadi leo shahidi huyo atakapoendelea kutoa ushahidi kutokana na wao kama jopo kupata dharura.

Mawaziri hao wa zamani kwa pamoja wanatuhumiwa kuingia mkataba na kuisamehe kodi kinyume cha sheria kampuni  ya  M/S Alex Stewart  Government  Bussines Cooparation, jambo linalodaiwa kuwa lilisababisha serikali kupata hasara ya Sh.11bilioni.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 .

Awali mchunguzi mkuu daraja la pili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Saddy  Kambona akitoa ushahidi dhidi ya kesi hiyo alidai kuwa kampuni hiyo ya Alex Stewart Government Business Cooperation ilipata msamaha wa kodi kwa tangazo la Serikali lililosainiwa na Mramba bila kufuata ushauri uliotolewa na TRA kuwa haikustahili kupata msamaha wa kodi.

Shahidi huyo wa 12 wa upande wa mashtaka aliendelea kudai kuwa Mramba licha ya kufahamu kuwa kulikuwa hakuna bajeti ya 2003/04 iliyoandaliwa kwa ajili ya malipo ya kampuni hiyo, alimuagiza Gavana wa Benki Kuu kusaini.

Baada ya kutoa hoja hizo, Wakili wa Mramba, Herbert Nyange alimhoji shahidi huyo kuwa hizo ndiyo zilikuwa sababu za kumfanya aamini kuwa kulikuwepo na mazingira ya rushwa?

Kambona alijibu kuwa mazingira hayo  yalimfanya aamini kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa makusudi na mahusiano.

Kambona aliongeza kudai kuwa hana la kusema kuhusu hoja kuwa Mramba anahusika katika uundwaji wa kampuni hiyo.

Alidai kuwa kampuni hiyo siyo miongoni mwa  kampuni zilizoshiriki na kupitishwa katika mchakato wa kumtafuta mzabuni wa ukaguzi wa dhahabu.

Kambona alidai kuwa M/S Alex Stewart ya Uingereza siyo miongoni mwa kampuni tano zilizoshiriki na kupitishwa wakati wa mzabuni wa kumtafuta mkaguzi wa madini ya dhahabu nchini Alex Assayers Limited  ya Uingereza, Alex Stuart Co. Ltd na Walker Whythe.

Akitoa ushahidi wake Septemba 4, mwaka huu, Kambona aliwasilisha vilelezo vinne vilivyonyesha kuwa mshtakiwa alikiri kuwa walivunja sheria.

Akitoa ushahidi wake, shahidi huyo alidai kuwa Mramba aliruhusu malipo ya awali kwa kampuni hiyo licha ya kujua kuwa mkataba ulikuwa haujasainiwa.

                                             CHANZO:MWANANCHI

No comments: