ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 7, 2010

Kondakta alivyouawa kikatili na polisi

Na Rashid Mkwinda, MbeyaPOLISI wawili kati ya saba waliofika katika eneo la tukio la mauaji ya kikatili ya kondakta wa mabasi ya Sumry, Revocatus Chisunga (32), (pichani), wanashikiliwa na jeshi hilo huku upelelezi juu ya tukio hilo ukiendelea.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, polisi hao wanashikiliwa kutokana na tukio la askari mmoja kumpiga risasi kichwani Chisunga iliyosababisha kifo chake katika Baa ya Twiga, mjini hapa hivi karibuni.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kuwa, uchunguzi unaendelea na kwamba atatoa maelezo baada ya kupata taarifa za uhakika.

Wiki iliyopita askari polisi wanaokadiriwa kufikia saba walifika katika baa na nyumba ya kulala wageni ya Twiga iliyopo Mabatini mjini hapa kwa lengo la kuwakamata watu waliodaiwa kutaka kumuibia mmoja wa wateja wa gesti hiyo.
Inadaiwa kuwa, katika kufanikisha hilo, maafande hao walifika kkwenye baa hiyo na kuingia kwa nguvu kisha kumlenga risasi ya kichwani Chisunga aliyekuwa akijipatia kinywaji eneo hilo.


Wakizungumza kutoka katika eneo la tukio, baadhi ya mashuhuda ambao hawakupenda kutaja majina yao walidai kuwa, askari hao walifika eneo hilo kufuatia taarifa za kuwepo kwa dalili za kufanyika uhalifu.

“Ndani ya ile gesti kulikuwa na mtu anayedaiwa kuwa, alikuwa na pesa nyingi na kwamba ilidaiwa kuna watu walikuwa wanachora ramani ya kumliza. Polisi walipopewa taarifa walifika aneo hilo na katika purukushani walimuua kijana wa watu aliyekuwa anakunywa kinywaji nje ya gesti hiyo.

“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha sana kwani kulikuwa na njia nyingine za kutumia kuweza kuwatia nguvuni wahalifu hao kama walikuwepo lakini kitendo cha wao kufanya mauaji yale, hakikuwa sahihi,”alidai mmoja wa wananchi hao.

Akiongea na Uwazi mmiliki wa baa hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Bilauri alisema kuwa, siku ya tukio akiwa nyumbani kwake saa 8.45 usiku alipigiwa simu na wahudumu wake na kuelezwa kuwa, polisi walifika katika eneo hilo na kumuua mmoja wa wateja.

“Ni kwamba kijana aliyeuawa alipowaona polisi wameingia aliinuka na kutaka kukimbia ndipo wakampiga risasi kichwani. Baada ya kupata taarifa hizo nilifika kwenye eneo la tukio na kumkuta yule kijana tayari amekufa huku akiwa na jeraha kichwani,”alisema Bilauri.

Naye Meneja wa Mabasi ya Sumry, Soud Salim alielezea kusikitishwa kwake na mauaji ya mfanyakazi wake huyo huku akishangaa madai ya kuhusishwa na ishu ya ujambazi.
Marehemu amezikwa katika Kijiji cha Laela Sumbawanga, ameacha mjane na watoto wawili.


                                                CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS 

No comments: