Mke wa aliyekuwa mwanamuziki mkongwe wa dansi nchini Tanzania, marehemu Ramazani Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’, Toni Ongala (pichani) ameugua ghafla na kupelekwa hospitalini baada ya kupata mshtuko kufuatia kifo cha mumewe, Risasi Jumamosi limeinyaka.
Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dar, Alhamisi iliyopita, mtoto mkubwa wa marehemu, Jessica Ongala alisema kuwa, mama yao ameugua ghafla siku tano tu tangu kumzika mumewe kipenzi.
Alisema kuwa, hali hiyo iliwapa mshtuko mkubwa watoto kiasi cha kuanza kumuomba Mungu apishie mbali baya lolote ndani ya familia hiyo.
“Kwa kweli mama anaumwa, anatapika, malaria pia, lakini zaidi amepata mshtuko na presha kwa kifo cha mumewe, sisi wenyewe tulichanganyikiwa, tukamuomba Mungu,” alisema Jessica.
Aliongeza kuwa, wao kama watoto, walimpeleka kwenye hospitali moja iliyopo Mbezi, Jijini Dar ambako aliandikiwa tiba ya kuchoma sindano moja kila siku kwa muda wa siku tano ili kusitisha kutapika na matatizo mengine.
Akaongeza: “Anachoma sindano moja kila siku, kidogo leo (Alhamisi) ana nafuu kwa mbali. Anaweza hata kuongea na kuachia tabasamu.”
Jessica anayeishi Dubai akifanya kazi ya ualimu, alisema kwa sasa mjane huyo wa marehemu anaishi kwa mtoto wake, Kalimangonga Ongala ‘Kally’, Mbezi, Jijini Dar.
Gazeti la Risasi Jumamosi linamtakia afya njema mjane wa marehemu Dk. Remmy Ongala, Toni Ongala katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Dk. Remmy alifariki dunia Desemba 13, mwaka huu kwenye hospitali ya Regency, Dar baada ya kupata matatizo ya kisukari na kiharusi.
Alizikwa Desemba 16, 2010 kwenye makaburi ya Sinza, Dar. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment