Mapenzi ni kanuni, ukijua kuhudumia, utahudumiwa!-2
Asilimia kubwa ya watu ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi, husumbuliwa na tatizo la kutotengeneza penzi. Wakiongozwa na msemo kuwa kila kitu hupangwa na Mungu, nao huacha mapenzi yao yaende kama yalivyo. Hawaamini kuwa barabara ilichongwa ndiyo magari yakapita.Ukiona vyaelea ujue vimeundwa! Hii inamaana kuwa kila kinachostawi, nyuma yake kuna ujenzi uliofanyika. Usimuone babu na bibi wanasherehekea miaka 50 ya ndoa yao ukadhani ni jambo lililokuja lenyewe. Kuna mambo ya msingi ambayo waliyafanya kuhakikisha wanadumu mpaka kuzikana.
Ukiwa mwingi wa hasira, matatizo yanayotokea hutaki kuyaweka mezani ili myajadili na kuyamaliza, kila siku utakuwa unabadili uhusiano. La! Hutobadili lakini utabaki kwenye penzi ambalo unaishi bila amani. Huna furaha! Ni mpenzi lakini hamfungamani, mnakuwa kama wapinzani wa jadi! Uhusiano bora ni ule ambao wanaoujenga ni watu makini na ambao wanajua nini ambacho wanakifanya. Wenye kufahamu thamani ya penzi lao na kila mmoja anaheshimu umuhimu wa mwenzake. Wanaoguswa kutoa chochote kuhakikisha wanaendelea kuwa bora kimapenzi.
Hii ndiyo sababu ya kukutaka uhangaike na ikiwezekana utumie gharama yoyote ili mwenzi wako awe na furaha. Utengeneze thamani yako kwake, kiasi kwamba akikuona aone mbele yake kasimama mtu aliyeishikilia dunia yake. Inawezekana! Mapenzi ni ujanja, utundu, kuguswa na kujitolea!
Huna sababu ya kushindwa kugharamia furaha ya mwenzi wako kwa sababu ukiacha gharama yake ni kubwa. Utakosa kila kitu muhimu ambacho mtu sahihi angependa kupata kutoka kwa mwenzi wake. Na hiyo itakusumbua! Kama hutafikiria, basi utaona kwa wengine na utatamani!
Hapa chini nakuchambulia hasara ambazo unaweza kukutana nazo kwa kushindwa kuhudumia furaha ya mwenzi wako;
UTAKOSA AMANI
Misongo (stresses) ya kimaisha inatesa. Inawezekana unafanya kazi sana. Wakati mwingine masuala ya kiofisi au biashara hayaendi kama inavyotakiwa. Unashinda siku nzima ukipigana kuhakikisha unasonga mbele. Iwe umeajiriwa, umejiajiri au umeajiri! Kichwa hakitulii mpaka unahisi ni kizito.
Kufikia hapo, bila shaka unahitaji faraja. Ni kipindi ambacho huhitaji mwenzi sahihi ili aweze kukusahaulisha matatizo ya kimaisha. Mtu ambaye anakujua ulivyo, kwahiyo inamuwia rahisi kutambua kwamba upo kwenye matatizo na kuchukua hatua zinazofaa kurekebisha hali.
Fikiria kwamba ukiwa katika hali hiyo, unarudi nyumbani ambako unakutana na moto mwingine. Amani hakuna! Kichwa chako kinaweza kuchanganyikiwa. Kama sivyo, maradhi ya moyo yatakunyemelea. Kupata kilicho bora, kiandae. Palilia shamba na ulilime kama unataka kuvuna.
Ukifanikiwa kumuweka mwenzi wako katika hali ya furaha, utapata faraja muda wote. Yakikufika, ukirejea nyumbani utakuta amani. Utakutana na tiba ya msongo wa mawazo ulionao. Hiyo ndiyo tafsiri ya upendo, kwahiyo usije kukosa utulivu wa moyo. Anza leo kumfurahisha ili naye akupe mahaba tele!
UTACHOKWA HARAKA
Hakuna kitu kibaya kwenye mapenzi kama mtu kuchokwa na mwenzi wake. Lakini hilo siyo zito, ni rahisi mno kama hutaamua kushughulikia kasoro ulizonazo.
Huna ubunifu, mwenzi wako haoni kitu chochote kipya. Mwenzi wako hana furaha, wewe hujishughulishi. Ataanza kukuona ni mzigo na mwisho wa siku atakuchoka. Usikubali hali hiyo ikutokee, anza leo! Maisha ya kimapenzi ni mazuri sana endapo utaamua.
MTASHINDWA KUJADILIANA
Mwenzi wako hana furaha, wewe unaingia mlango huu naye anapitia ule. Hayo ni maisha mabaya mno! Mnapatwa na mambo ambayo mngependa kushauriana, lakini mnashindwa kufanya hivyo kwasababu mnaishi kama Simba na Yanga.
Kuna watu wanaishi kwa kalamu, wanalala mzungu wa nne! Kama matumizi, yanawekwa mezani, akitaka kutoa agizo anaandika ‘kimemo’ na kukiacha juu ya stuli! Hawaguswi kutafuta furaha yao, hawataki kuzungumza na kumaliza tofauti zao.Matokeo yake ni siri za ndani kuzagaa mitaani. Hili likikufika ni sawa na msiba. Chukua hatua!
HUTAPATA HUDUMA BORA
Mwenzi wako anahitaji kuwa na furaha ili aweze kukupa huduma bora. Amini kwamba yeye ndiye anaweza kukufanya hii dunia uione yote ni yako. Changamka leo!
Unahitaji huduma bora kutoka kwa mwenzi wako, na hilo anaweza kulitimiza endapo atakuwa na furaha dhidi yako. Hii inamaana kwamba kuanzia sasa, punguza maudhi kwa mwenzi wako na umzidishie amani. Akupende na amini ndani ya nafsi yake kwamba wewe ndiye mtu bora zaidi maishani mwake.
Ukimfurahisha, atakupa huduma bora ambayo huwezi kuipata popote. Bila shaka atakapokuhudumia, nawe utajiona umepata mwenzi sahihi wa maisha yako. Hayo ndiyo mapenzi. Yakistawishwa hustawi! Mapenzi ni kanuni, ukihudumia utahudumiwa.
No comments:
Post a Comment