Ofisa Mtendaji wa TTCL, Amir Said,akikabithi msaada kwenye vituo vya watoto yatima ili kuwawezesha watoto hao,kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL), imetoa msaada wa simu za mezani, mbuzi na vyakula kwa vituo vinne vya watoto yatima ili kuwawezesha watoto hao,kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Msaada huo wenye thamani ya Sh5 milioni, ulikabidhiwa na Ofisa Mtendaji wa TTCL, Amir Said, kwa viongozi na wawakilishi wa vituo hivyo.
Katika hotuba yake fupim, ofisa mtendaji huyo, alivitaja vituo vilivyopewa msaada huo kuwa ni Mama Theresa cha Mburahati, Yatima Group, Kituo cha yatima cha Kibaha na kile cha Mkakuya.
Amir alisema kila kituo kimepewa simu moja ya mezani yenye muda wa maongezi wenye thamani ya Sh 100,000 kwa ajili ya mawasiliano ya kiofisi.
Pia alisema, kila kituo kimepewa mbuzi mmoja na vyakula mbalimbali ukiwemo mchele na sukari, ili kuwawezesha watoto hao kuungana na wenzao duniani, katika kusherehekea sikukuu.
"Wakati tunasherehekea sikukuu hizi ni vyema tukawakumbuka wenzetu ambao hawana uwezo wa kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, ndiyo maana tumeamua kuwapa msaada huu ili nao washerehekee kwa furaha," alisema.
Alisema kampuni hiyo itaendelea kusaidia jamii yenye mahitaji muhimu kila inapopata uwezo wa kufanya hivyo.
Kiongozi wa kituo cha Mkakuya, Cecilia Ngarinje, alisema ukosefu wa chakula ni tatizo kubwa katika kituo hicho.
Alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto yatima katika kituo hicho hali inayosababisha uendeshaji wake kuwa mgumu kutokana na mahitaji makubwa ya chakula.
"Ni vigumu kuwakataa watoto yatima wasiokuwa na walezi kujiunga na kituo chetu. Lakini ingawa tunawakubali, uendeshaji wa kituo na hasa katika masuala ya chakula, unakuwa mgumu," alisema.
Aliziomba taasisi nyingine za serikali na za watu binafsi kuvisaidia vituo vya watoto yatima ili viweze kuendesha shughuli za kuwasaidia watoto yatima kwa ufanisi zaidi.
Mlezi wa kituo cha Yatima Group, Haruna Mkandika, aliushukuru uongozi wa TTCL kwa uamuzi wa kuwapa msaada huo na kuahidi kuutumia kwa lengo lililokusudiwa.
"Tunashukuru kwa msaada wa simu, itatusaidia kuwasiliana na taasisi nyingine ambazo ni wadau wa kituo chetu kwa ajili uendeshaji wa kituo,"alisema.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment