ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 7, 2010

Wassira: Tuko tayari kukaa mezani na Chadema

Mr Wasira
Sadick Mtulya
SERIKALI imesema iko tayari kukaa meza moja na chama cha upinzani cha Chadema au taasisi nyingine yoyote itakayotaka kujadiliana kuhusu mustakabali wa taifa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira alisema kuwa serikali iko tayari kwa mazungumzo hayo iwapo yataweka mbele maslahi ya taifa.
Kauli ya Wassira imetolewa wakati Chadema ikiendelea na msimamo wake wa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi wa urais, ikitaka kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza utangazaji wa matokeo hayo; kuandikwa kwa katiba mpya na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.


Chadema, ambayo ilitangaza msimamo huo mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu, ilithibitisha kwa vitendo kauli hiyo wakati wabunge wake walipotoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kukihutubia chombo hicho.
Baadaye, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kuwa chama hicho kiko tayari kukaa meza moja na serikali au taasisi yoyote kujadili suala hilo kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Lakini katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alibeza kauli hiyo ya Mbowe kwa kusema kuwa chama hicho tawala hakina muda wala sababu ya kuketi pamoja na wapinzani hao na kwamba baada ya rais kupatikana, siasa sasa zinahamia bungeni.

Jana Waziri Wassira alitoa kauli tofauti na ya katibu wake mkuu alipoiambia Mwananchi kuwa wako tayari kukaa meza moja na Chadema, chama au taasisi yoyote ikiwamo za dini na kwamba mazungumzo watayoyalenga ni yale yatakayohakikisha yanaweka mbele maslahi ya taifa.
“Lakini nasisitiza serikali haina mgogoro na viongozi wa dini au chama chochote bali milango ipo wazi kwa vyama vyote 18 na taasisi zote," alisema waziri huyo ambaye aliwahi kuwa kwenye upinzani baada ya kuihama CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi miaka ya tisini.

"Majadiliano yasichukue sura ya kisiasa au udini kwa kuwa kufanya hivyo hakutafanikisha kufikiwa kwa  maslahi bora ya baadaye ya nchi.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha taifa hili linalifikishwa mahali ambapo amani na utulivu itaendelea kuwepo.”
Hata hivyo, Waziri huyo alisema kama kutatokea matatizo au kutoelewana, serikali ina njia na taratibu zake inazozitumia kukutana na walengwa kutatua hali hiyo na kwamba hatua hizo huwa hazitangazwi kwenye vyombo vya habari.

Wakati akifafanua msimamo huo wa Chadema kwa waandishi wa habari, Mbowe alisema mazungumzo watakayoyalenga ni yale yatakayohakikisha kuwa madai yao yanafikiriwa kwa kina huku maslahi ya taifa yakiwekwa mbele.
Mbowe alisema wanafurahi kuona kuwa kitendo chao cha kutoka bungeni wakati wa hotuba ya Rais Kikwete kimesaidia kuibua mjadala mzito nchini ambao iwapo utapewa nafasi ya kujadiliwa bila kuweka ushabiki wa kisiasa, nchi inaweza kupata mabadiliko makubwa siku za usoni.

Alitoa mfano kauli ya waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na Jaji Mkuu Augustino Ramadhani ambao walikaririwa wakisema kuwa suala la katiba mpya ni muhimu.
“Maoni kama haya, ambayo yanatoka kwa watu wazito kama hawa, yanaonyesha kuwa kitendo chetu kimeamsha mjadala wa maana kwa taifa hili,” alisema.
Chadema, ambayo ilionekana kama haingesimamisha mgombea urais baada ya Mbowe kuamua kugombea ubunge wa Jimbo la Hai, iliibukia kuwa mpinzani mkuu wa CCM baada ya kumtangaza mbunge wa zamani wa Karatu, Dk Willibrod Slaa kuwa mgombea urais.

Dk Slaa, ambaye alikuwa akivutia maelfu ya watu kwenye mikutano yake ya kampeni ambako alikuwa akihubiri elimu ya bure na upunguzaji wa bei za vifaa vya ujenzi, alitangaza kutokubaliana na mwenendo wa utangazaji matokeo ya uchaguzi wa rais na kuitaka Tume ya Uchaguzi (Nec)kusimamisha zoezi hilo.
Lakini Nec iliendelea na utangazaji matokeo na baadaye kumtangaza Jakaya Kikwete kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais, tamko ambalo liliifanya Chadema kutangaza msimamo wake wa kutotambua matokeo ya uchaguzi wa rais

                      CHANZO:MWANANCHI

No comments: