ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 26, 2011

Aliyeongoza kidato cha nne ni yatima

Lucylight Mallya
Mussa Juma, Arusha
 
MWANAFUNZI aliyeongoza mtihani wa kidato cha mne kitaifa mwaka 2010, Lucylight Mallya (18), amebainika kuwa ni yatima ambaye wazazi wake wote walifariki dunia miaka minne iliyopita.
 
Akizungumza katika mahojiano maalum, akiwa nyumbani kwa baba yake mkubwa kijiji cha Nguruma wilayani Arumeru, binti huyo aliyekuwa akisoma katika Shule ya Sekondari ya Marian, iliyoko Bagamoyo, mkoani Pwani alisema anamshukuru Mungu, walimu na walezi wake kwa kumwezesha kufaulu.
 
"Sikutegemea kuwa wa kwanza namshukuru sana Mungu, walimu, walezi wangu hasa baba mkubwa na mama na wote walionifikisha hapa ikiwa ni pamoja na wanafunzi wenzangu....," alisema Lucylight.
 
Lucylighty ambaye ni kwanza kati ya watoto, wanne walioachwa na marehemu wazazi walofariki dunia mwaka 2006 na (2007), alisema malengo yake ni kuwa daktari.
 
Binti huyo alisema wakati anafanya mtihani huo, somo aliloona gumu lilikuwa ni fizikia, lakini anamshukuru Mungu kuwa amefaulu vizuri na kuwa wa kwanza hapa nchini.
 
"Mimi nilikuwa napenda sana Kemia, Bailojia na Fizikia na nilikuwa nimejiandaa sana hivyo namshukuru Mungu kunisaidia kutimiza ndoto zangu," alisema Lucylighty.
 
Baba Mkubwa wa Lucy ambaye ndiye anamlea, Dominick Mallya alisema anashukuru Mungu kwa binti yake huyo kuongoza kitaifa.
 
Hata hivyo, Mallya alisema binti huyo amesoma katika mazingira magumu kwasababu hakuwa na fedha za kutosha hivyo alimwomba mmiliki wa shule hiyo, Father Valentine Bayo kumtafutia mfadhili.
 
"Mamshukuru Father Bayo kwani tangu mtoto huyu akiwa kidato cha pili hadi kumaliza kidato cha nne alikuwa analipiwa na wafadhili,"alisema Mallya.
 
Hata hivyo, aliomba wafadhili wa kumsaidia, ili aweze kuendelea ya masomo ya kidato cha tano hadi sita na chuo kikuu kwasababu yeye (Mallya) hanafedha za kutosha kuwasomesha watoto wote alionao.
 
"Baba yake Lucy ambaye ni mdogo wangu alifariki dunia mwaka 2006  na mkewe alifariki mwaka 2007, waliacha watoto wanne na mimi nina watoto watano hivyo tunashindwa kumudu gharama za kuwasomesha," alifahmisha Mallya na kuongeza:
 
“Tungependa kupata tena ufadhili wa Lucylight ili aweze kuendelea na masomo ya juu katika shule ambayo alikuwa akisoma”.
 
Lucylight alizaliwa Jijini Dar es Salaam, miaka 18 iliyopita alisoma Shule ya Msingi St Mary's Tabata na baada ya  alihitimu la saba mwaka 2006 alichaguliwa kwenda Shulea ya Sekondari ta Wasichana Tabora lakini aliamua kwenda Marian Girls alikohitimu kidato cha nne mwaka jana.
 
Taarifa za maendeleo yake zinaonyesha kuwa akiwa kidato cha kwanza alishika nafasi ya tatu, lakini kuanzia kidato cha pili hadi cha nne alikuwa akishika nafasi ya kwanza.

No comments: